WAKATI kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kikiwa kimewasili tokea jana mjini Dodoma, mshambuliaji hatari wa timu hiyo, Mbaraka Yusuph, ameweka wazi kuwa kila mchezo wanaoingia dimbani kwao ni kama fainali.

Kikosi hicho kimewasili mkoani humo kikiwa la lengo moja tu kuhakikisha kinaibuka na ushindi dhidi ya wenyeji wao, Singida United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma keshokutwa Jumamosi saa 10.00 jioni.

Mshambuliaji huyo ameonekana kuendelea na kasi yake ya ufungaji aliyokuwa nayo msimu uliopita alipokuwa Kagera Sugar kufuatia kufunga mabao mawili katika mechi mbili mfululizo za Azam FC na kuiwezesha timu hiyo kuibuka na pointi zote tatu.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Yusuph alisema wanajua ya kuwa kila mchezo wanaocheza unakuwa mgumu kutokana na timu pinzani kuwakamia, lakini amedai malengo yao ni kushinda kila mtanange.

“Kwanza namshukuru Mungu kucheza mechi hizi salama pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kufunga pia napenda sana kujitahidi kadiri ya uwezo wangu kila mechi niwe naweza kufunga ili niweze kuweka rekodi nzuri katika msimu huu na nawaahidi mashabiki kuwa mfungaji bora,” alisema.

Akizungumzia mchezo ujao dhidi ya Singida United, Yusuph alisema kuwa; “Kwa kweli mechi yoyote ile Azam ikikutana na timu yoyote mechi inakuwa ngumu kwa vile watu wanakuwa wanakamia sana, kauli mbiu yetu kila mechi sisi kwetu fainali tunapambana ili tuweze kufunga.”

Azam FC ikiwa mkoani hapa Dodoma imefikia katika Hoteli ya African Dreams Conference Centre, ambapo mara ya kuwasili jana ilifanya mazoezi mepesi kwenye maeneo ya hoteli hiyo na leo Alhamisi jioni inatarajia kufanya mazoezi ya kwanza kuelekea mtanange huo unaotarajia kuwa mkali na wa aina yake.