BEKI kisiki wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Yakubu Mohammed, ametwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa timu hiyo (NMB Player Of The Month) mwezi Agosti mwaka huu.

Mohammed anayeunda safu ya ulinzi ya Azam FC ambayo ndio pekee mpaka sasa ambayo haijaruhusu wavu wake kuguswa tokea Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ilivyoanza Agosti 26 mwaka huu, ametwaa tuzo baada ya kupendekezwa na kupigiwa kura nyingi na mashabiki wa soka kwenye mitandao ya kijamii ya timu hiyo.

Wachezaji wengine wa Azam FC wanaounda safu hiyo bora ya ulinzi ni beki mwingine kisiki Agrey Moris, kipa Razak Abalora, Daniel Amoah na Bruce Kangwa huku wakishirikiana vema na safu imara ya kiungo chini ya Nahodha Himid Mao ‘Ninja’, Stephan Kingue, Frank Domayo na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Tuzo hiyo inatolewa na mdhamini mkuu wa Azam FC, Benki bora nchini kwa sasa ya NMB kwa usalama wa fedha zako, ambapo itatolewa leo Jumapili kabla ya kuanza mchezo wa timu hiyo dhidi ya Lipuli ya Iringa saa 1.00 usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Twaha aibuka kidedea Azam B

Aidha kiungo wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Azam FC (Azam B), Twaha Hashir Rajab, ameibuka kidedea kwa kunyakua tuzo hiyo kwa upande wa wachezaji vijana inayoitwa Uhai Player Of The Month, inayotolewa na mdhamini namba mbili wa mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu uliopita..

Rajab, 16, amekuwa na kiwango kizuri tokea alipojiunga na kikosi hicho akitokea Bom Bom Acdemy msimu huu.