KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo asubuhi kimeanza rasmi mazoezi kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Lipuli ya Iringa.

Mtanange huo utafanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Jumapili hii Septemba 24 saa 1.00 usiku.

Wachezaji wote wa Azam FC wamerejea mazoezini isipokuwa kipa Benedict Haule, anayesumbuliwa na majeraha ya kidole gumba chake akiungana na majeruhi wengine wa muda mrefu Joseph Kimwaga na Shaaban Idd.

Mara baada ya kumalizia programu ya mazoezi mepesi asubuhi, Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, ataendelea na programu nyingine ya mazoezi leo jioni yote ni katika kuwatengeneza vilivyo wachezaji kuelekea mtanange huo.

Hadi inaelekea kwenye mchezo huo, kikosi cha Azam FC bado kimeendeleza rekodi yake nzuri ya kutopoteza mechi yoyote huku ikiwa ni miongoni mwa timu mbili ambazo hazijaruhusu wavu wake kuguswa, nyingine ikiwa ni Simba.

Kwa mujibu wa msimamo wa ligi, Azam FC inashika nafasi ya tatu ikiwa imejikusanyia pointi saba sawa na Simba, ambayo iko juu yake kwa tofauti ya mabao ya kufunga huku Mtibwa Sugar ikiwa kinara kwa pointi zake tisa ilizojikusanyia.