NAHODHA wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’, ameweka wazi kuwa kwa sasa hawaangalii kuwa juu au chini kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Mao amesema kwa sasa wanaangalia malengo ya klabu ya kuuchukulia uzito mchezo hadi mchezo huku akijinasibu ya kuwa watajipanga vema kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mtanange ujao dhidi ya Lipuli utakaofanyika Septemba 23 mwaka huu.

“Kwanza tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kushinda mchezo (vs Kagera jana) na kupata pointi tatu muhimu, lakini kuwa juu au chini sidhani kama ni kitu cha msingi sana kwa sasa, kwa sababu malengo ya timu ni kuuchukulia uzito mchezo baada ya mchezo.

“Tumeshinda mchezo wa leo tunamshukuru Mwenyezi Mungu tu, tunatazama mchezo unaokuja tupate matokeo mazuri pia, cha kwanza ni ushindi ukizingatia timu yetu ina wachezaji wengi wapya karibia asilimia 50, kwa hiyo sio kitu kizuri sana kuwapa presha kubwa ya kufunga mabao mengi au kupata matarajio makubwa katika kipindi hiki ni kuwapa muda kwani wachezaji wengine ni wadogo kabisa,” alisema Himid mara baada ya mchezo huo.

Bao pekee la Azam FC kwenye mchezo huo limefungwa na Mbaraka Yusuph akitumia vema pasi maridadi ya kinda mwingine Yahya Zayd, ambaye naye alipenyezewa pasi ya kukata na Idd Kipagwile.

Hilo ni bao la pili kwa Yusuph kuifungia Azam FC tokea ajiunge nayo msimu huu, linguine akitupia kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Transit Camp iliyochapwa mabao 8-1, pia akiwa ameifunga timu yake zamani aliyoichezea msimu uliopita kabla ya kutua kwa mabingwa hao Juni mwaka huu.

Azam FC inayodhaminiwa na maji safi kabisa ya Uhai Drinking Water, Benki bora ya NMB na Tradegents, inatarajia kuendelea na mazoezi keshokutwa Jumatatu asubuhi kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Lipuli ya Iringa utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumamosi ijayo kuanzia saa 1.00 usiku.