KESHOKUTWA Ijumaa saa 1.00 usiku, Uwanja wa Azam Complex utawaka moto pale, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC itakapokuwa ikiwania pointi tatu muhimu itakapopiga na Kagera Sugar kwenye mchezo namba 17 wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Tayari kikosi cha Azam FC kinachodhaminiwa na Maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki ya NMB na Kampuni ya Tradegents, kimeshaanza maandalizi tokea Jumatatu kujiandaa na mchezo huo, ambao kama wakishinda wanatarajia kukaa kwa mara ya kwanza kileleni mwa msimamo wa ligi msimu huu wakifikisha pointi saba.

Mchezo huo unatarajia kuwa mkali na wa aina yake, hasa ikizingatiwa Kagera Sugar iliibuka na ushindi kwenye mchezo wa mwisho wa ligi msimu uliopita baina ya timu hizo, uliofanyika katika dimba hilo na kuifanya timu hiyo kupoteza jumla ya mechi tatu kihistoria tokea Azam Complex ufunguliwe Agosti 20 mwaka 2011.

Aidha mshambuliaji mpya wa Azam FC, Mbaraka Yusuph, kama akicheza mchezo huo atakuwa akicheza mechi yake ya kwanza dhidi ya timu yake ya zamani, aliyoichezea msimu uliopita kabla ya kujiunga na matajiri hao wa viunga vya Azam Complex msimu huu.

Azam FC itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kutopoteza mchezo tokea msimu huu uanze, pia kwa ubora mkubwa wa kutoruhusu wavu wake kuguswa, ikiwa imeifunga Ndanda bao 1-0 na kutoka suluhu na Simba wikiendi iliyopita.

Kagera Sugar inayonolewa na Mecky Mexime, yenyewe bado haijakuwa na mwenendo mzuri tokea msimu huu uanze, kwani katika mechi mbili walizocheza imefanikiwa kuvuna pointi moja tu baada ya kutoka sare ya 1-1 na Ruvu Shooting huku ikipoteza mchezo wa kwanza kwa kufungwa na Mbao bao 1-0, zote zikichezwa nyumbani kwake Uwanja wa Kaitaba.

Rekodi muhimu (2008-2017)

Wakati timu hizo zikienda kupambana, huo utakuwa ni mchezo wa 19 kihistoria tokea zianze kukutana Ligi Kuu, katika mechi 18 zilizopita, Azam FC imeonekana kuwa na wastani mzuri ikiwa imeshinda mara tisa, ikipoteza mara tano huku michezo minne ikiisha kwa sare.

Katika mechi saba zilizopita dhidi ya Kagera Sugar, Azam FC imeonekana kufanya vizuri baada ya kushinda mara sita huku Kagera Sugar ikishinda mchezo mmoja tu, jambo ambalo linawapa nafasi nzuri zaidi mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu uliopita, kuibuka kidedea kwenye mchezo ujao.

Mechi zote walizocheza VPL    

20/05/17       Azam FC        0-1    Kagera Sugar (L) 

28/10/16       Kagera Sugar  2 – 3  Azam FC (W)

08/05/16             Kagera Sugar  1 – 2  Azam FC      (W)

27/12/15       Azam FC  2 – 0   Kagera Sugar (W)

18/04/15       Azam FC  2 – 1   Kagera Sugar (W)

20/01/15       Kagera Sugar 1 – 3  Azam FC       (W)

02/02/14     Azam FC   4 – 0   Kagera Sugar (W)   

14/09/13      Kagera Sugar   1 – 1   Azam FC (D)

26/01/13      Azam FC  3 – 1  Kagera Sugar      (W)

15/09/12             Kagera Sugar   0 – 1   Azam FC (W)

06/05/12      Azam FC   2 – 1   Kagera Sugar (W)

30/10/11             Kagera Sugar   0 – 0   Azam FC (D)

15/01/11      Azam FC   1 – 2   Kagera Sugar  (L)

15/09/10       Kagera Sugar   1 – 0   Azam FC  (L)   

18/01/10      Azam FC   1 – 1   Kagera Sugar  (D)   

23/08/09      Kagera Sugar   3 – 2   Azam FC  (L)

14/04/09       Kagera Sugar   1 – 1   Azam FC  (D)

18/10/08       Azam FC   1 – 2   Kagera Sugar (L)

*Azam FC: Win : 9, Draw : 4, Lose : 5