KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aristica Cioaba, amesema kuwa kumuingiza kiungo Frank Domayo, kuliifanya timu hiyo kumiliki mpira kipindi cha pili dhidi ya Simba.

Mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ulifanyika jana Jumamosi jioni kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, jijini Dar es Salaam na kuisha kwa suluhu.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Cioaba alisema timu zote mbili ziligawana vipindi, akidai Simba ilimiliki kipindi cha kwanza huku kwa upande wao wakimiliki kipindi cha pili baada ya kumuingiza Domayo na kumpumzisha winga Enock Atta Agyei.

“Ninafuraha kubwa Simba kuja kucheza uwanja wetu wa nyumbani umeona ni mchezo wa kiungwana (fair play), wamecheza na mechi imekuwa nguvu sawa, ingewezekana Azam FC kushinda au Simba kushinda.

“Napenda kusema kuwa dakika 45 za kipindi cha kwanza, Simba waliweza kumiliki eneo la kiungo nilikuwa na tatizo kwenye eneo langu la kiungo na umiliki wa mpira ulikuwa mkubwa kwa Simba, lakini tulikuwa na nafasi mbili hadi tatu za kuweza kufunga mabao,” alisema.

Cioaba alisema kuwa kipindi cha pili aligundua tatizo kwenye kikosi chake na kuamua kumuingiza Domayo na kujitahidi kushinda mchezo huo lakini ilishindikana.

“Huu ni mpira na umeisha kwa sare, ninafuraha kubwa kwa matokeo lakini sijafurahishwa na namna tulivyocheza na nilikuwa na matatizo mawili kwenye mchezo huo,” alisema.

Kikosi cha Azam FC kinachodhaminiwa na maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki bora ya NMB na Kampuni ya Tradegents, kwa sasa kinashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi kwa pointi zake nne sawa na Simba, Yanga, Lipuli na Tanzania Prisons, ambazo ziko juu yake kutokana na tofauti ya uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa huku Mtibwa Sugar iliyoshinda mechi zake zote mbili ikiwa kileleni kwa pointi sita.

Baada ya kupata mapumziko ya siku moja leo Jumapili, kikosi hicho kinatarajia kuanza rasmi mazoezi kesho Jumatatu jioni kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Kagera Sugar utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Ijumaa ijayo Septemba 15 mwaka huu saa 1.00 usiku.