NAHODHA wa Klabu Bingwa ya  Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’, amewaambia mashabiki wa timu hiyo wajitokeze kwa wingi Jumamosi ili kushuhudia ushindi watakaoupata dhidi ya Simba.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu uliopita hivi sasa wanaendelea na maandalizi makali kuelekea mtanange huo, ambao kwa mara ya kwanza utapigwa ndani ya uwanja huo ukianza saa 1.00 usiku.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi, Mao alisema maandalizi yao yanaendelea vizuri huku akidokeza kuwa wachezaji wenzake wote wana morali kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

“Mimi cha kuwaambia mashabiki waje kwa wingi waje waisapoti timu kwa ajili ya sisi tuweze kushinda mchezo,” alisema.

Kiungo huyo anayesifika kwa ukabaji wa hali ya juu, anayemudu kucheza nafasi zote za ulinzi isipokuwa langoni, aliongeza kuwa morali yao imeongezeka zaidi kutokana na mchezo huo kupigwa nyumbani ndani ya viunga vya Azam Complex.

“Daima maandalizi yanakuwaga mazuri kwa ajili ya kushinda mchezo haijalishi mnacheza na nani, lakini maandalizi yanakuwaga mazuri zaidi ya mechi zote tunazochezaga hapa nyumbani yaani watu wanakuwaga na morali wanakuwaga na ari kwa sababu wanajua mara nyingi tumekuwaga na matokeo mazuri sana katika uwanja huu.

“Kwa hiyo hiko ndio kitu kizuri kinatupa moyo sisi wachezaji, na hata washabiki inabidi waje waisapoti timu kwa ajili ya kuja kushuhudia ushindi tutakaoupata,” alisema.

Kocha naye anena 

Kwa upande wake Kocha Msaidizi wa Azam FC, Idd Nassor Cheche, alisema kuwa mchezo huo wanauchukulia umuhimu licha ya kuwa ni kama michezo mingine wanayocheza kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

“Huu ni mchezo wetu wa pili wa ligi na tunahakikisha tunacheza nyumbani na uwanja wetu wa nyumbani tunataka tushinde kwa sababu toka tumefungua uwanja wetu huu tumewahi kupoteza mara tatu tu na hatutegemei kupoteza tena katika msimu huu.

“Kwa hiyo kwanza ni kitu cha umuhimu kwamba tuweze kushinda nyumbani, halafu mwaka huu tuna dhamira ya kufanya mambo makubwa zaidi,” alisema.

Cheche alisema kuwa ushindani ni mkubwa kikosini hali ambayo inawapa wakati mgumu wao kama makocha katika kukipanga kikosi hicho.

“Morali ni kubwa…wakati fulani inatupa wakati mgumu kufikiria nani nimweke wapi na nani nimweke wapi kwa sababu kila mtu ana hamu nayo, sasa hii inatupa kazi rahisi kwamba yule atakayepata nafasi ya kuanza atatupa yale mategemeo ambayo tunatarajia sisi,” alisema.

Safu ya ushambuliaji yaboreshwa

Kutokana na safu ya ushambuliaji kupoteza nafasi nyingi kwenye mchezo wa kwanza walioifunga Ndanda bao 1-0, Cheche ameweka wazi kuwa tayari wameshalifanyia kazi ikiwemo pia kuhakikisha safu zote zinakuwa imara katika mtanange huo.

“Mchezo wa mpira ulivyo ni mchezo wa makosa, hauwezi kuwa bora kila siku, tumeanza vizuri katika safu ya ulinzi na kiungo, matatizo katika ushambuliaji na sasa hivi tumelifanyia kazi sana hilo na kuhakikisha na yale tuliyofanya nyuma katika kiungo na ulinzi yasije yakabadilika, kwa hiyo tumehakikisha idara zote zinakaa vizuri ili kutupa matokeo mazuri katika michezo yetu kuanzia huu na mingine inayokuja mbele,” alisema.

Rekodi VPL

Huo utakuwa ni mchezo wa 19 kwa timu hizo kukutana Ligi Kuu tokea Azam FC ianze kucheza VPL msimu wa 2008/2009 ilivvyopanda daraja, ambapo katika mechi 17 zilizopita Azam FC ikiwa imeshinda mara sita na Simba mara nane huku mechi nne zikiwa zimeisha kwa sare.