KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, jioni hii imeichapa Transis Camp mabao 8-1 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, aliutumia mchezo huo kama sehemu ya kuwaweka kwenye ushindani wachezaji wake ikiwamo kukiangalia kiufundi kabla hakijacheza na Simba Jumatano ijayo katika mtanange wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Azam FC iliyofanikiwa kuutawala mchezo wote katika kila kipindi ikicheza soka safi na kutumia vikosi viwili tofauti, ilijipatia mabao yake kupitia kwa Yahaya Mohammed aliyefunga mawili dakika ya 22 kwa njia ya penalti na dakika ya 23 akimalizia krosi safi ya Bruce Kangwa.

Kangwa aliipatia bao la tatu Azam FC dakika ya 45 baada ya ya kuwazidi maarifa mabeki wa Transit na kuingia eneo la 18 kabla ya kupiga shuti lilomshinda kipa na hivyo kuifanya timu hiyo kumaliza kipindi cha kwanza ikiwa na uongozi wa mabao 3-0.

Kipindi cha pili Azam FC ilianza kwa kubadilisha kikosi kizima, ambacho kiliingia na kasi mpya na kufanikiwa kufunga mabao matano yaliyohitimisha ushindi huo mnono.

 Alikuwa ni winga Enock Atta Agyei, aliyeichachafya vilivyo ngome ya ulinzi ya Transit Camp baada ya kufunga mabao matatu peke yake yaani ‘hat-trick’ akifunga dakika ya 50, 78 na 89.

Mshambuliaji mpya wa Azam FC, Mbaraka Yusuph, naye alifungua akaunti ya mabao kwa kufunga bao lake la kwanza tokea ajiunge na timu hiyo, akilitupia wavuni dakika ya 67 akimalizia mpira uliotemwa na kipa kufuatia shuti kali la Enock Atta.

Bao jingine la Azam FC lilifungwa dakika ya 72 na Joseph Mahundi kwa kichwa akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na winga Idd Kipagwile, aliyeonyesha kiwango kizuri akitengeneza mabao matatu katika mchezo huo.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitaendelea tena na mazoezi kesho Jumamosi jioni tayari kabisa kuiwinda Simba katika mchezo ujao wa ligi utakaofanyika Uwanja wa Uhuru Septemba 6 mwaka huu.

Kikosi cha Azam FC leo:

Razak Abalora/Benedict Haule dk 46, Daniel Amoah/Swalehe Abdallah dk 46, Bruce Kangwa/Hamimu Abdulkarim dk 46, Yakubu Mohammed/Abdallah Kheri dk 46, Agrey Moris (C)/David Mwantika, Frank Domayo/Salmin Hoza dk 46, Braison Raphael/Joseph Mahundi dk 46/Abdul Omary dk 69, Salum Abubakar/ Abdallah Masoud dk 46, Yahaya Mohammed/Mbaraka Yusuph dk 46, Yahya Zayd/Enock Atta dk 46, Ramadhan Singano/Idd Kipagwile dk 46