KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kesho Ijumaa inatarajia kukipiga dhidi ya Transit Camp, katika mchezo wa kirafiki unaotarajia kufanyika Uwanja wa Azam Complex kuanzia saa 10.00 jioni.

Mchezo huo ni maalum kabisa kwa ajili ya benchi la ufundi la Azam FC chini ya Kocha Mkuu Aristica Cioaba, kuwaweka katika ushindani wachezaji wake kutokana na wikiendi hii kutokuwa na mchezo wowote wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Aidha atautumia pia kama sehemu ya kukisoma kikosi chake kabla ya kuvaana na Simba Jumatano ijayo katika mchezo wa ligi, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Kikosi cha Azam FC kipo kwenye hali nzuri na morali ya hali ya juu kuelekea mtanange huo muhimu, ambapo wachezaji wanaari kubwa ya kuzoa pointi zote tatu kwa ajili ya kujenga heshima na kujiweka sawa kwenye mbio za ubingwa wa ligi.

Katika mchezo wa kwanza wa ligi, Azam FC inayodhaminiwa na maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki bora ya NMB na Tradegents, ilishinda ugenini mkoani Mtwara kwa kuichapa Ndanda ya huko bao 1-0, lililofungwa kwa kichwa na mshambuliaji Yahaya Mohammed, akimalizia mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Bruce Kangwa.