USHINDI wa bao 1-0 ilioupata Azam FC katika mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) juzi dhidi ya Ndanda, umeifanya kujiongezea rekodi kadhaa tokea ipande daraja mwaka 2008.

Pointi hizo tatu zimeifanya Azam FC kuanza ligi ikiwa nafasi ya nne kwenye msimamo, ambapo inazidiwa kwa uwiano wa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya timu zilizo juu yake za Mwadui, Tanzania Prisons na Simba iliyoko kileleni, zote zikiwa na idadi hiyo ya pointi.

Rekodi ya kwanza waliyoandikisha Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati, ni ya kuvuna ushindi wa sita kwenye mechi za ufunguzi wa ligi kati ya mechi 10 ilizocheza tokea ianze kucheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu wa 2008-2009.

Ni mara nne tu ambazo Azam FC ilitoka uwanjani bila kuvuna ushindi katika mechi ya kwanza ya ufunguzi, mara mbili ikifungwa (Azam FC 2-3 Moro United, Kagera Sugar 3-2 Azam FC) na sare mbili (Mtibwa Sugar 1-1 Azam FC, Azam FC 1-1 African Lyon).

Kwa mujibu wa takwimu, miongoni mwa mechi nane zilizofanyika katika wiki ya kwanza ya ligi zilizojumuisha timu 16 zinazoshiriki, Azam FC ni moja ya timu saba zilizoonja ushindi, huku pia ikiwa ni miongoni mwa timu tano zilizoanza ligi bila kuruhusu wavu wake kutikiswa.

Mechi nyingine moja iliyobakia, iliisha kwa sare, ambapo ilishuhudiwa Lipuli ya Iringa iliyokuwa ugenini ikilazimishwa sare ya bao 1-1 na Yanga.  

Rekodi Nangwanda

Bao pekee lililofungwa na Yahaya Mohammed, limeifanya Azam FC kuandikisha ushindi wa pili ndani ya Uwanja wa Nangwanda Sijaona kihistoria tokea Ndanda ilivyoanza kucheza Ligi Kuu msimu wa 2014-2015, mara ya kwanza kupata ushindi ilikuwa ni msimu wa 2015-2016, mabingwa hao wakiibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Shomari Kapombe kwa kichwa kufuatia krosi ya Kipre Tchetche.

Kiujumla umekuwa ni ushindi wa tano katika mechi zote nane walizokutana (mara nne kwenye ligi na moja kwenye Kombe la FA), timu hizo zimetoka sare mara moja huku Azam FC ikipoteza mara mbili zote zikiwa ugenini ndani ya uwanja huo.

Yahaya Mohammed, anaungana na Shaaban Idd kuwa washambuliaji pekee wa Azam FC waliofunga mabao mawili katika mechi zote walizocheza dhidi ya Ndanda, bao la kwanza Yahaya aliloifunga timu hiyo ilikuwa ni mechi ya pili ya msimu uliopita walipopata ushindi kama huo.

Shaaban kwa upande wake ambaye kwa sasa ni majeruhi, mabao hayo mawili aliifunga timu hiyo kwenye mechi moja ya Kombe la FA (Azam Sports Federation Cup) katika ushindi wa 3-1, bao jingine likiwekwa kimiani na Ramadhan Singano ‘Messi’.