BODI ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) imefanya marekebisho kadhaa kwenye ratiba ya ligi hiyo, yaliyogusa mechi nne za Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC.

Mabadiliko hayo yamefanyika kutokana na mechi za timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, ambazo zipo kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Wikiendi hii Septemba 2, Stars itakuwa kibaruani kumenyana na timu ya Taifa ya Botswana, ukiwa ni mchezo wa kimataifa wa kirafiki utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Kutokana na mchezo huo, umeilazimu bodi hiyo kuusogeza mbele mchezo wa Azam FC iliyokuwa ikitarajiwa kucheza na Simba Jumamosi ijayo, ambapo hivi sasa mtanange huo utapigwa Septemba 6 mwaka huu.

Mechi zingine zitakazofanyika siku hiyo ambazo zimesogezwa mbele, ni kati ya Tanzania Prisons na Majimaji ya Songea, Njombe Mji na  Yanga, Mtibwa Sugar na Mwadui FC, Lipuli itamenyana na Stand United, Singida United ikiivaa Mbao, Kagera Sugar itaialika Ruvu Shooting wakati Mbeya City ikicheza na Ndanda FC.

Mechi nyingine za Azam FC zilizopanguliwa ni ile itakayowakutanisha dhidi ya Kagera Sugar, iliyokuwa ipigwe Septemba 9 na sasa itafanyika Septemba 11 mwaka huu, mchezo unaotarajiwa kuwa wa kwanza kwa mabingwa hao kuutumia uwanja wake wa nyumbani wa Azam Complex msimu huu.

Mchezo mwingine wa Azam FC dhidi ya Mbao, uliotarajiwa kupigwa Oktoba 7 kwenye Uwanja wa Kirumba Mwanza, sasa umepangiwa tarehe nyingine, ambapo utafanyika Oktoba 11 mwaka huu.

Novemba 15 mwaka huu, Azam FC itakuwa ugenini ndani ya Uwanja wa Kambarage, Shinyanga kukipiga na Stand United, awali mchezo huo ulipangwa kufanyika Novemba 11.

Mechi nyingine zilizoguswa

Septemba 21 mwaka huu Mbao itakipiga na Tanzania Prisons, Oktoba 11 utashuhudiwa mtanange kati ya wenyeji Kagera Sugar watakaoivaa Mwadui, Mbeya City wataonyeshana kazi na Ruvu Shooting huku Ndanda ikiumana na Singida United.

Njombe Mji wataialika Simba Oktoba 11, sawa na Mtibwa Sugar wakaoivaa Tanzania Prisons, Lipuli watakipiga na Majimaji huku Oktoba 12 Stand United ikitarajia kumenyana na Yanga.

Mechi nyingine za Novemba 15 mwaka huu, Mbao itacheza na Yanga; Kagera na Mbeya City; Mwadui na Ruvu Shooting; Singida na Njombe Mji; Lipuli na Tanzania Prisons; Mtibwa Sugar na Majimaji wakati Novemba 16, Ndanda itacheza na Simba.