KOCHA Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, ameonyesha furaha yake kubwa kwa wachezaji wake kufuatia hali ya kupambana waliyoonyesha uwanjani jana na kufanikiwa kuzoa pointi tatu dhidi ya Ndanda.

Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup), walizoa pointi zote tatu katika mchezo huo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kuichapa Ndanda bao 1-0 ugenini ndani ya Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara lililofungwa kwa kichwa na Yahaya Mohammed.

Cioaba ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co,tz kuwa licha ya uwanja kuwa mbovu kikosi chake kiliweza kucheza kwa umoja, kwa nguvu na kudai ni jambo zuri liloanza kuonekana kwa manufaa ya baadaye.

“Ni jambo zuri kushinda mchezo wa kwanza, siku zote mchezo wa kwanza unakuwa mgumu, dakika 45 za kwanza niliweza kuutawala mchezo na kutengeneza nafasi tatu hadi nne za wazi za kufunga mabao, kupitia kwa Yahya Zayd, Yahaya Mohammed, kama wangefunga bao la pili na hakika matokeo yangekuwa zaidi ya mabao mawili au matatu.

“Kipindi cha pili wachezaji wangu waliendelea kucheza lakini uwanja ulikuwa kikwazo kikubwa kutokana na ubovu, kama uliiona Azam FC ilikuwa ikitaka kucheza soka zuri kwa kumiliki mpira, lakini ilionekana kuwa tatizo kila walipofanya hivyo,” alisema.

Aidha Kocha huyo wa zamani wa Aduana Stars ya Ghana, aliwashukuru mashabiki wa Azam FC waliosafairi kutoka mbali kwa ujumla wao na wengine, kwa ajili ya kuisapoti vilivyo timu hiyo katika mchezo huo.

Kuelekea mechi na Simba

Cioaba alisema kuwa hivi sasa kikosi chake kina muda mrefu wa wiki moja kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Simba huku akidai kuwa malengo ya timu hiyo ni kukusanya pointi nyingi kadiri iwezekanavyo kwenye mechi zote watakazocheza.

“Simba ni moja ya timu nzuri wanacheza mpira mzuri, na sasa tunasuri kitakachotokea kwenye mchezo huo, timu yangu (Azam FC) malengo yake hivi sasa katika kila mchezo ni kuwa makini na kukusanya pointi nyingi kadiri iwezekanavyo,” alisema.

Kwa Azam FC kuanza na ushindi jana ni dalili njema ya kufanya vizuri msimu huu, kwani msimu uliopita katika mechi ya ufunguzi ilitoka sare ya nyumbani ya bao 1-1 dhidi ya African Lyon.

Kikosi hicho tayari kimerejea jijini Dar es Salaam leo Jumapili mchana, ambapo kwa mujibu wa programu ya locha huyo kesho wachezaji wote watapumzika kabla ya kuendelea na mazoezi keshokutwa Jumanne jioni isipokuwa wachezaji wawili, nahodha Himid Mao ‘Ninja’ na kipa Mwadini Ally, watakaoenda kuripoti kwenye kambi ya timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars inayojiandaa na mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Botswana Jumamosi ijayo.