KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeanza na ushindi kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuunya Vodacom Tanzania (VPL) baada ya kuichapa Ndanda bao 1-0, katika mtanange uliomalizika jioni hii ndani ya Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Bao pekee la Azam FC limefungwa na mshambuliaji raia wa Ghana, Yahaya Mohammed, dakika ya 36 kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na beki wa kushoto Bruce Kangwa.

Hilo ni bao la pili Yahaya kuifunga Ndanda, la kwanza alifunga msimu uliopita kwenye mchezo wa raundi ya pili ya ligi baada ya kupokea pande safi kutoka kwa nahodha Himid Mao ‘Ninja’.

Azam FC ilionyesha kuwa imedhamiria kupata pointi tatu katika mchezo huo, baada ya kulishambulia mfululizo lango la Ndanda kwenye dakika za awali za mchezo huo na kukosa mabao dakika ya 3, 4 na 5 kupitia kwa Yahaya na Yahya Zayd.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, alitumia mfumo wa 3-4-3, ambao ulionekana kufanya vizuri kwenye mchezo huo, mabeki wa kati Yakubu Mohammed, Aggrey Moris na Daniel Amoah wakionekana kukaba kwa nidhamu, wakisaidiwa na viungo wawili wa ukabaji Frank Domayo na Stephan Kingue.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu uliopita, walifanikiwa kwa kiasi kikubwa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga mabao katika kila kipindi, lakini zilishindwa kutumiwa vema.

Aidha katika mchezo huo, Azam FC pia iliutumia kutambulisha jezi zake mpya itakazozitumia msimu huu, ambapo waliitumia ile ya ugenini yenye rangi ya bluu na mistari ya rangi nyeupe.

Pia ilifanikiwa kuwatumia wachezaji wake, kipa Razak Abalora, mshambuliaji Mbaraka Yusuph, aliyeingia kipindi cha pili, huku beki wa kushoto Hamimu Karim, Wazir Junior wakiwa benchini.

Mara baada ya kumalizika mchezo huo, kikosi hicho kinatarajia kurejea jijini Dar es Salaam, kesho alfajiri tayari kabisa kuanza maandalizi ya mchezo wa pili wa ligi dhidi ya Simba.

Kikosi kilikuwa hivi:

Razak Abalora, Agrey Moris, Yakubu Mohamed, Daniel Amoah, Bruce Kangwa, Himid Mao, Stephan Kingue/Enock Atta dk 89, Frank Domayo, Salum Abubakar, Yahya Zayd/Braison Raphael dk 83, Yahaya Mohammed/Mbaraka Yusuph dk 55