KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kimeanza safari leo Jumatano saa 12 asubuhi kuelekea mkoani Mtwara, tayari kabisa kuanza rasmi msimu wa 2017-2018 wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa kuvaana na Ndanda.

Mchezo huo utafanyika Jumamosi ijayo Agosti 26 mwaka huu katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, ambapo kikosi hicho kimeondoka kikiwa kamili kuuanza vema msimu mpya, isipokuwa mshambuliaji Shaaban Idd, aliyeko nchini Afrika Kusini kwa matibabu ya majeraha ya misuli ya nyonga na kiungo Salmin Hoza, ambaye naye ni majeruhi.

Msimu uliopita timu hizo zilipokutana, Ndanda ilishinda mabao 2-1 ndani ya uwanja huo, bao pekee la Azam FC ilikifungwa na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Francisco Zekumbawira, lakini ikalipa kisasi kwa kuifunga bao 1-0 ndani ya Dimba la Azam Complex.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu uliopita, wanaodhaminiwa na Benki bora nchini ya NMB, Maji safi ya Uhai Drinking Water na Tradegents, pia msimu uliopita waliwasukuma nje Wanakuchele hao katika robo fainali ya michuano ya Kombe la FA (Azam Sports Federation Cup) kwa kuwanyuka mabao 3-1. mabao mawili yakifungwa na Shaaban Idd na jingine likiwekwa kimiani na Ramadhan Singano ‘Messi’.