MSHAMBULIAJI mpya wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Wazir Junior, ameweka wazi kuwa yupo tayari kwa mapambano.

Junior amedai kuwa moja ya malengo yake ni kuisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu ujao.

“Kuanza kwa msimu mpya 2017-2018, kwangu mimi nimejipanga kuisaidia timu yangu kuwa mabingwa msimu ujao na mwenyewe kucheza vizuri kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu kwani ushirikiano wetu ndio utatupa hamasa kama wachezaji ya kufanya vizuri na kuisaidia timu yetu kubeba ndoo (ubingwa),” alisema Junior wakati akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz

Junior ni mmoja wa washambuliaji wanaokuja kwa kasi kwa sasa nchini, amesajiliwa Azam FC msimu huu akitokea Toto African ya Mwanza aliyoifungia mabao saba msimu uliopita.

Azam FC inatarajia kufungua msimu mpya wa ligi Jumamosi ijayo Agosti 26 mwaka huu kwa kukipiga dhidi ya Ndanda, mtanange unaotarajia kufanyika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Kuingia haraka kwenye mfumo

Junior ni mmoja wa wachezaji wapya wa Azam FC walioingia kwa haraka kwenye mfumo wa timu hiyo akiwa amefanya vizuri kwenye mechi za majaribio za maandalizi ya msimu (pre season) kwa kufunga mabao mawili, amedai kuwa hiyo imetokana na kusikiliza kwa makini maelekezo ya kocha.

“Ni kufuata tu maelekezo ya kocha anayotaka na wewe kujiamini kile ambacho unakifanya unajua ukiwa unajiamini unakuwa unafanya kitu ambacho mwalimu naye anakipenda, lakini ukiwa haujiamini kwa kile unachofanya unahisi utakosea hiyo ipo kwenye mpira lakini mimi nimefuata maagizo ya mwalimu na nikafanya kitu ambacho ninacho, ndio kimenisaidia kufanya vizuri,” alisema.

Changamoto ya kupigania namba

Ushindani wa namba kwenye eneo la ushambuliaji la Azam FC analocheza Junior, umeonekana kuwa mkubwa kukiwa na takribani wachezaji watano wengine baadhi yao wakiwa ni Yahya Zayd, Yahaya Mohammed, Mbaraka Yusuph, Shaaban Idd, hilo halimpi shida straika huyo baada ya kuweka wazi kuwa hilo linatarajiwa kuamuriwa na kocha.

“Mwalimu ndio anayejua mwenyewe huyo acheze lakini kucheza kwa vipi, unapofanya vizuri katika mazoezi na kwenye mechi ukipata nafasi hata dakika tano unavyozitumia, ndio mwalimu anakuamini na kukupa dakika nyingine zinazokuja kwa hiyo changamoto ipo tu tutapigana nayo.

“Lakini kikubwa ni ushirikiano kwa sababu mimi siwezi kuchukua mpira golini mpaka golini ili niende nikatupie (nikafunge), lakini lazima tusaidizane, pasi inatoka hapa inakwenda sehemu nyingine, inakuja kwangu nampa mtu mwingine halafu tunafunga na tunasonga,” alisema.

Ushirikiano ni mkubwa kitimu 

“Ushirikiano kitimu ni mkubwa na tukiendeleza hivi naamini msimu huu hamna timu ambayo itatubabaisha, tukicheza kitimu kama hivi na kupendana ndani na nje ya uwanja, tukiondoa ule utofauti basi sisi ndio mabingwa msimu ujao, mashabiki wetu wawe na morali kwamba sisi tunakuja kivingine, tunakuja kubeba ndoo (ubingwa) msimu ujao 2017-2018,” alisema.

Ufungaji, uchezaji bora

Kila mchezaji hakosi kujiwekea malengo binafsi wa kufikia mafanikio fulani, kwa upande wake Junior amesema kuwa amejipanga kupambana kwa kugombea tuzo mbili binafsi za kuwa mfungaji bora na mchezaji bora msimu ujao.

“Ni kutupia tu (kufunga mabao) na kugombea uchezaji bora na ufungaji bora eeeh!, ufungaji bora msimu huu hata nisipopata mimi apate mchezaji ambaye anatoka kwenye timu yangu itakuwa ni jambo zuri,” alisema.

Jambo linalompa matumaini kujipa matarajio hayo makubwa ni kutokana kikosi hicho kilivyokuwa vizuri kufuatia usajili wa wachezaji wengi wenye vipaji na umri mdogo bila kungalia majina waliosajiliwa.

“Timu ipo vizuri wachezaji wote wapo vizuri, kwa hiyo timu ikiwa na wachezaji wazuri na wewe ukiwa mzuri basi unakuwa unacheza vizuri, kwa hiyo matumaini yapo na wachezaji wenzangu wapo vizuri kwa hiyo tutashirikiana na kikubwa ni ushirikiano hakuna kingine,” alisema.

Utofauti anaouona kwa mashabiki

“Mashabiki wa Azam FC kuna kitu wanataka tofauti na timu ndogo, yaani malengo ya timu ndogo ni kutoshuka daraja lakini malengo ya timu kubwa kwa mashabiki ni kubeba ndoo, kwa hiyo mashabiki wa Azam watarajie ndoo (ubingwa) msimu ujao kwa kutupa sapoti nje na ndani ya uwanja,” alisema

Aliongeza kuwa: “Mashabiki wa Azam FC waje uwanjani na waje kwa wingi kwenye mechi yetu na Ndanda, kwa sababu ndio mechi yetu ya kwanza waje watushangilie na sisi tunaonyeshe kuwa hatuwaangushi, mimi nawakaribisha kwenye mechi zote za Azam wasiwe na kinyongo waje wakiwa wanajiamini wakijua wanakuja kuburudika na sio kuhuzunika na kuja kuifurahia timu yao mpya.”

Mshambuliaji huyo aliyepata majeraha ya kuchanwa na vipande vya chupa juu ya mguu wa kushoto na kushinwa nyuzi moja wakati Azam FC ikiwa nchini Uganda wakati ikielekea kucheza na Onduparaka, iliyoifunga mabao 3-0, tayari anaendelea vizuri akiwa ameanza rasmi mazoezi mepesi tokea juzi Ijumaa tayari kujiandaa na mchezo huo muhimu.

Kuelekea mchezo huo dhidi ya Ndanda, msafara wa Azam FC unatarajia kwenda mkoani Mtwara Jumatano ijayo wakiwa kamili kabisa kuandikisha ushindi katika mchezo wake huo wa kwanza wa ligi.