KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aristica Cioaba, ameweka wazi kuwa mechi tano za kirafiki alizocheza nchini Uganda, zimempa mwelekeo namna atakavyokipanga kikosi chake kuelekea msimu ujao.

Azam FC imemaliza kambi ya siku 10 nchini humo jana kwa mafanikio makubwa bila kupoteza mchezo wowote, baada ya kuichapa Vipers bao 1-0, mechi nyingine nne ilizocheza imetoka sare ya 2-2 na timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ ya wachezaji wa ndani (CHAN), ikakipiga tena na mabingwa wa nchi hiyo KCCA na kutoka sare ya 1-1.

Mechi nyingine mbili zilizobaki iliweza kuibuka kidedea kwa kuzichapa URA (2-0), na ikainyuka Onduparaka mabao 3-0, mechi zote zikiwa maalumu kwa ajili ya msimu ujao, ambapo Azam FC itashiriki michuano mitatu, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Kombe la Mapinduzi na Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo huo, Cioaba alisema mechi hizo tano zimekuwa na umuhimu mkubwa kwa kikosi chake katika kuwapa mbinu wachezaji, huku akidai zimemsaidia kutengeneza kikosi cha kwanza.

“Mechi hizi tano zimekuwa na umuhimu kwenye kikosi changu, kwa wachezaji kusikiliza mbinu, kujenga morali yao, na hatujapoteza mchezo wowote na tunarejea Tanzania kwenda kumalizia maandalizi ya mwisho ya ligi,” alisema.

Aukubali ushindani

Ciaoba alisema amefurahishwa sana na aina za mechi ambazo timu yake imecheza nchini humo kutokana ushindani mkubwa ulioonyeshwa kwenye mechi zote, akidai ni kitu kizuri kwa kikosi chake katika kipindi hiki cha maandalizi.

“Niliamua kuja hapa kutokana na kufahamu kuwa soka la Uganda lipo juu, na nilijua ya kuwa nitapata mechi nyingi za nguvu, mechi zote zilikuwa zinaonyeshwa kwenye televisheni, nimechukua DVD zote na nitaangalia mimi na benchi langu kuona ni jambo gani lilikuwa zuri kwenye mechi, na lipi baya, tukisharejea Dar es Salaam nitafanya uchambuzi na kurekebisha makosa.

“Najua nina mechi ya kwanza ugenini ya ligi (Ndanda), nina muda wa siku tisa za maandalizi, nitaangalia ni kitu gani cha muhimu cha kufanya mazoezini, ninafuraha kubwa kuja hapa Uganda na sijapoteza mchezo wowote na ninarudi nyumbani wachezaji wangu wakiwa na morali nzuri,” alisema.

Wakati huo huo, kikosi hicho jioni ya leo Jumanne kimerejea jijini Dar es Salaam, tayari kabisa kufanya maandalizi ya mwisho kabla ya kuanza rasmi mikikimikiki ya ligi, inayotarajia kuanza kutimua vumbi Agosti 26 mwaka huu.

Mara baada ya kurejea, kikosi hicho kimepewa mapumziko ya siku mbili kesho Jumatano na Alhamisi na kitaanza rasmi mazoezi Ijumaa ijayo saa 10.00 jioni.