KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, jioni ya leo imemaliza kambi yake ya siku 10 nchini Uganda kwa kuichapa Vipers bao 1-0 mchezo uliofanyika Uwanja wa St, Mary’s, Kitende, Uganda.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, aliendelea na mfumo wake wa kubadilisha kikosi kwa kuwapa nafasi wachezaji wote kucheza, baada ya kuingiza kikosi kipya katika mchezo huo tofauti na kile kilichoanza jana kwenye ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Onduparaka.

Bao pekee la Azam FC kwenye mchezo huo uliokuwa mkali na nguvu, lilifungwa na mshambuliaji Yahya Zayd, kwa njia ya mkwaju wa penalty dakika ya 29 kufuatia winga Joseph Mahundi, kuangushwa ndani ya eneo la hatari.

Mara baada ya mchezo huo, uongozi wa Vipers chini ya mmiliki wake na Rais, Lawrence Mulindwa, uliialika Azam FC chakula cha jioni kama sehemu ya kujenga mahusiano na kuishukuru kwa kufika Uganda.

Katika sehemu ya maongezi yake, Mulindwa, ambaye ni Rais Mstaafu wa Shirikisho la Soka Uganda, aliipongeza kiujumla Kampuni ya Azam, kwa udhamini waliouweka kwenye Ligi Kuu Uganda huku akiitakia kila kheri Azam FC itwae ubingwa wa ligi msimu ujao sambamba na timu yake.

Ikiwa nchini Uganda, Azam FC imefanikiwa kucheza mechi tano kali za kirafiki za maandalizi ya msimu ujao kwa mafanikio, ikianza kwa kutoka sare ya mabao 2-2 na Uganda ‘The Cranes’, ikaambulia sare nyingine ya bao 1-1 dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu Uganda (Azam Uganda Premier League) KCCA.

Mechi tatu za mwisho, ilizinyuka URA mabao 2-0 kabla ya kuzichapa Onduparaka na leo hii Vipers, iliyoshika nafasi ya tatu kwenye ligi hiyo msimu uliopita.

Baada ya kuhitimisha ziara hiyo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam kesho Jumanne saa 7 mchana, tayari kabisa kumalizia maandalizi ya mwisho ya ligi, itakayoanza kutimua vumbi Agosti 26 mwaka huu, Azam FC ikianzia ugenini kwa kukipiga na Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Kikosi cha Azam FC leo:

Benedict Haule, Swalehe Abdallah/Himid Mao dk 57, Hamimu Karim/Bruce Kangwa dk 68, Abdallah Kheri, David Mwantika, Salmin Hoza, Joseph Mahundi/Frank Domayo dk 60, Braison Raphael, Yahya Zayd/Joseph Kimwaga dk 46, Ramadhan Singano/Masoud Abdallah dk 46, Idd Kipagwile/Salum Abubakar dk 78