MSHAMBULIAJI mpya wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Mbaraka Yusuph, ameahidi kuibuka mfungaji bora wa michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) inayotarajia kuanza kutimua vumbi Agosti 26 mwaka huu.

Yusuph aliyesaini mkataba wa miaka miwili ni miongoni mwa washambuliaji wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao akitokea Kagera Sugar alikofunga mabao 12 msimu uliopita na kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora Chipukizi.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Mbaraka alisema kuwa anafuraha kujiunga na Azam FC na kudai alikuwa na ndoto ya muda mrefu kujiunga na miamba hiyo ya soka Afrika Mashariki na Kati.

“Kwa kweli nimejipanga kufanya vizuri zaidi kuliko msimu uliopita, natarajia Mwenyezi Mungu akinijalia kila mechi nitakayocheza niweze kupata nafasi, niweze kufunga na kuwa mfungaji bora wa ligi,” alisema Yusuph.

Mshambuliaji huyo aliyeko kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, hakusita kuisifia Azam FC akisema kuwa amefurahishwa na namna inavyojali wachezaji wake.

“Kufika Azam FC ni njia moja ya mimi kusonga mbele, hivyo nina mpango wa kucheza soka la kulipwa katika timu kubwa zaidi, ila hauwezi kwenda kucheza huko bila kujituma mazoezini pamoja na kwenye mechi, nina imani nitafika huko,” alisema.

Yusuph ambaye anavutiwa na staa wa Baracelona na Argentina, Lionel Messi, amewapa ahadi mashabiki wa Azam FC ya timu hiyo kufanya vizuri msimu ujao huku akiwaoamba waisapoti zaidi timu hiyo.

Hivi sasa straika huyo hatari mwenye spidi na uwezo wa kupachika mabao, yupo kambini nchini Uganda pamoja na wachezaji wa timu hiyo akiendelea na programu ya mazoezi mepesi kufuatia kutoka kwenye majeraha na anatarajia kuanza rasmi mazoezi ya ushindani na wenzake wiki ijayo.