KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (Azam FC) inaendelea na kambi yake nchini Uganda, tayari imejulikana programu ya mechi tatu za kirafiki itakazocheza nchini hapa.

Azam FC iliyowasili nchini humu jana, inatarajia kukaa kwa takribani siku 10 Uganda ikifanya maandalizi ya mwisho kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Kwa mujibu wa programu hiyo, Azam FC itaanza mchezo wa kwanza wa kirafiki Agosti 10 mwaka huu ikicheza na KCCA kwenye Uwanja wa Phillip Omondi jijini Kampala.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu uliopita, watashuka tena dimbani Agosti 13 kukipiga na Onduparaka ndani ya dimba hilo hilo.

Ziara hiyo itahitimishwa Agosti 14 mwaka huu kwa Azam FC kukipiga na Vipers kabla ya kuanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam, Tanzania siku inayofuata.

Awali Azam FC ilitakiwa kucheza mechi nyingine URA na SC Villa lakini kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu, mechi hizo zimeshindwa kuthibitishwa hadi sasa.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, anaamini kikosi chake kitanufaika vilivyo kwa kuimarika na kuwa imara kwa msimu ujao kufuatia kambi hiyo ya siku 10 nchini humo.

Kikosi hicho kinatarajia kuendelea na programu yake ya mazoezi kwa siku ya pili leo jioni ili kujiweka sawa kabisa kabla ya mechi hizo na maandalizi kamili ya kuelekea msimu ujao.

Wakati huo huo, winga wa Azam FC Ramadhan Singano ‘Messi’, leo usiku anatarajia kuungana na wachezaji wenzake kambini nchini humo akitokea Dar es Salaam.

Jumamosi iliyopita, Messi aliongeza mkataba wa miaka miwili kuendelea kusalia kwa matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.