UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, unayofuraha kukutaarifu kuwa umefikia makubaliano na Yanga kuhusu usajili wa beki Gadiel Michael.

Kwa muda mrefu Yanga imekuwa ikionyesha nia ya kumsajili beki huyo, lakini haikuwahi kuja kufanya mazungumzo kwa ajili ya kuuvunja mkataba wake unaomalizika Desemba mwaka huu.

Tunashukuru viongozi wa Yanga wamekuwa waungwana na kuamua kufika leo kwenye ofisi zetu wakiongozwa na Mwenyekiti wa Usajili, Hussein Nyika, na hatimaye baada ya mazungumzo tukafikia muafaka kwenye suala hilo.

Hivyo baada ya pande zote kukubaliana ni rasmi sasa, tunathibitisha ni ruksa kwa Yanga kumsajili Gadiel kwa msimu ujao na tunamtakia kila la kheri katika maisha yake mapya ndani ya timu hiyo.

Azam FC ni timu inayoendeshwa kiueledi haiwezi kumbania mchezaji yoyote kuondoka kusaka malisho bora kama taratibu za usajili zimefuatwa.

Wakati huo huo, leo tumefanikiwa kuingia mkataba mpya wa miaka miwili na nyota wetu Ramadhan Singano ‘Messi’, ambaye mkataba wake wa awali ulifikia umefikia ukingoni.