NI buku mbili tu! Hiko ndio kiingilio rasmi kitakachokupa fursa ya kuishuhudia Azam FC ikitesti mitambo yake mipya ya msimu ujao kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam kesho Ijumaa, pale itakapokipiga dhidi ya KMC katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex kuanzia saa 10.00 jioni.

Azam FC imeshacheza mechi nne za maandalizi za kujiandaa na msimu ujao, lakini zote zikifanyika nje ya jiji la Dar es Salaam, hivyo ni nafasi pekee kwa mashabiki wa Azam FC na wengine kiujumla waishio jijini humo kuweza kuishuhudia timu hiyo.

Mbali na kiingilio hicho cha Sh. 2,000 kwa majukwaa ya kawaida, mashabiki watakaokaa kwenye majukwaa ya watu maalumu (V.I.P) watalipia Sh. 3,000 tu.

Tayari nyota wapya waliosajiliwa na Azam FC kwa  msimu ujao wamesharipoti kambini kuanza maandalizi, baadhi ya wachezaji hao ni makipa Benedict Haule na Razak Abalora, mabeki Saleh Abdallah, Hamimu Abdul, kiungo Salmin Hoza, Idd Kipagwile, Wazir Junior huku Mbaraka Yusuph akiendelea na programu maalumu baada ya kutoka kwenye majeruhi.

Benchi la ufundi la Azam FC chini ya Kocha Mkuu Aristica Cioaba, linatarajia kuutumia mchezo huo kama sehemu ya kukipima kikosi hicho kwa mara ya mwisho kabla ya kuondoka nchini Jumapili ijayo kwa ajili ya kuweka kambi ya siku 10 nchini Uganda itakapocheza mechi nyingine nne kali za kirafiki na kurejea Dar es Salaam Agosti 15 mwaka huu.

Awali katika mechi nne za kwanza za kirafiki zilizofanyika nje ya Dar es Salaam, Azam FC iliichapa Lipuli ya Iringa mabao 4-0, ikatoka suluhu na Mbeya City kabla ya kufungwa na Njombe Mji 2-0, mechi zilizofanyika Nyanda za Juu Kusini huku ule uliopigwa nchini Rwanda dhidi ya mabingwa wa nchi hiyo Rayon Sports, ikiteleza tena kwa kufungwa 4-2.

Tayari ratiba ya ligi hiyo imeshatoka wiki kadhaa zilizopita, ambapo Azam FC inayodhaminiwa na maji safi ya Uhai yaliyokuja na mwonekano mpya pamoja na Benki bora ya NMB, imepangwa kuanzia ugenini kwa kukipiga na Ndanda ya Mtwara, mtanange utakaofanyika Uwanja wa Nangwanda Sijaona Agosti 26 mwaka huu.