KIPA mpya wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Razak Abalora, ameweka wazi kuwa anaimani timu yake hiyo mpya itatwaa taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu ujao.

Abalora amejiunga rasmi na timu hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita akitokea WAFA SC ya nchini kwao Ghana, akiwa amesaini mkataba wa miaka mitatu wa kuwatumikia matajiri hao wa viunga vya Azam Complex.

Akifanya mahojiano maalumu na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kipa huyo amedai kuwa hayo ndiyo malengo yake kwa wakati huu kuhakikisha timu hiyo inatwaa taji hilo la ligi, inayotarajia kuanza Agosti 26 mwaka huu.

“Ni jambo zuri sana kujiunga na Azam FC, nilijisikia vizuri sana niliposikia wananitaka hivyo nataka kumshukuru Mungu kwa kunipa nafasi hii ya kujiunga na familia hii nzuri,” alisema.

Kilichomvuta Azam FC

Huwa ni jambo gumu sana kwa mwanasoka kuhamia kwenye ligi asiyoifahamu vizuri, lakini hili halikumuogopesha Abalora, ambaye ameeleza kuwa anaijua vizuri Azam FC kupitia kwa marafiki zake wanaoichezea timu hiyo.

“Yeah, naijua vizuri Azam FC, unajua baadhi ya marafiki zangu wako hapa, Yakubu Mohammed ni rafiki yangu niliongea naye mengi sana na akaniambia mambo mengi mazuri kuhusu klabu, hivyo nikasema kwa nini isiwe, nikasema ndiyo na kuja kujiunga na familia hii nzuri,” alisema.

Alivyojipanga na changamoto

Moja ya matamanio makubwa ya mchezaji yoyote anayetaka kufikia mafanikio, ni kuweza kuzikabili changamoto za nje na ndani ya uwanja, kuhusiana na hilo kipa huyo ameeleza kuwa atafanya kazi kwa bidii na kuhakikisha anaweka rekodi ya kutofungwa bao lolote (cleansheet) katika mechi 14 au 15 za msimu.

“Unajua hii ni changamoto mpya kwangu, jambo nililopanga ni kufanya kazi kwa bidii na kuthibitisha kwa mashabiki wa Azam FC kuwa niko hapa kwa ajili ya kuisaidia timu kufikia malengo yake, hivyo nimepanga pia kuendeleza rekodi ya kukusanya ‘cleansheet’ na nitakuwa na furaha kama nitaweza kufanya hivyo katika mechi 14 au 15 za msimu,” alisema.

Kipa huyo aliyekuwa akidaka katika kikosi cha pili cha timu ya Taifa ya Ghana ‘Black Stars’, kilichokuwa kwenye harakati za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) mwakani nchini Kenya, hadi anaondoka nchini Ghana alikuwa ameiongoza WAFA kutoruhusu bao katika 12 kati ya 22 alizodaka za Ligi Kuu Ghana.

Utofauti ndani ya Azam FC

“Kila kitu kipo vizuri kwa ujumla, miundombinu mizuri, ni timu iliyojipanga vizuri, kila kitu kipo safi na vizuri, ina kocha mwenye uzoefu (Aristica Cioaba), najisikia furaha sana kujiunga na familia hii nzuri,” alisema wakati akiizungumzia Azam FC akitofautisha na huko alipotoka.

Anamfuata Neuer

Abalora alisema anafuata nyayo za kipa bora kabisa kwa sasa duniani, Mjerumani Manuel Neuer, anayechezea Bayern Munich, ambapo amekuwa akijifunza kupitia kwake kila siku.

Mashabiki Azam FC

Mbali na kujitokeza uwanjani kuisapoti timu hiyo, kipa huyo aliwaomba pia mashabiki wa Azam FC kuiombea timu yao huku akidai watajitahidi kufanya vizuri kwa ajili yao.

Tayari ratiba ya ligi hiyo imeshatoka wiki kadhaa zilizopita, ambapo Azam FC inayodhaminiwa na maji safi ya Uhai yaliyokuja na mwonekano mpya pamoja na Benki bora ya NMB, imepangwa kuanzia ugenini kwa kukipiga na Ndanda ya Mtwara, mtanange utakaofanyika Uwanja wa Nangwanda Sijaona Agosti 26 mwaka huu.