KATIKA kuzidi kukiweka sawa kikosi kabla ya kuanza msimu ujao, Klabu Bingwa ya Afrika Masharikia na Kati, Azam FC, inatarajia kujipima na KMC FC Ijumaa ijayo, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Mchezo huo utakuwa ni wa mwisho kabisa wa Azam FC kabla ya kuelekea kwenye kambi ya siku 10 nchini Uganda Jumapili hii.

Meneja wa mabingwa hao aliuthibitishia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa mchezo huo ni maalum kwa kabisa kwa ajili ya kukiweka fiti kikosi hicho.

“Wote tunafahamu ya kuwa msimu unakaribia kuanza na baada ya mechi hiyo wachezaji watakuwa na mapumziko mafupi kwa saa kadhaa, halafu tarehe 6 tutakuwa na safari yetu ya kuelekea Uganda panapo majaaliwa kwenye mechi nyingine nne za kirafiki.

“Hiyo yote ni katika kuijenga timu na mwalimu kutengeneza kikosi chake cha kwanza na kujaribu kutafuta nani anafiti sehemu gani na nani anafiti kucheza na nani,” alisema Alando.

Kuelekea mchezo huo, kikosi cha Azam FC kimeendelea na mazoezi yake leo asubuhi mara mbili saa 1 na saa 3 huku kikitarajia kufanya kwa mara ya tatu jioni ya leo, yote ni katika kufanya maandalizi mazuri kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Azam FC inayodhaminiwa na maji safi kabisa ya Uhai yaliyokuja na mwonekano mpya, pamoja na Benki bora ya NMB tayari imepangwa kufungua pazia la ligi kwa kucheza na Ndanda Agosti 26 mwaka huu mchezo utakaofanyika Uwanja wa Nangwanda Sijaona.