UONGOZI wa Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, unayofuraha kuwataarifu kuwa umefikia makubaliano ya kuwatoa kwa mkopo wa msimu mzima wachezaji wake sita kwenye timu mbalimbali za Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL).

Wachezaji hao ni kipa Metacha Mnata anayekwenda Mbao pamoja na mshambuliaji Sadallah Mohamed, anayetokea kituo cha kukuza vipaji cha Azam FC, huku mabeki wawili Godfrey Elias maarufu kama Albino na Abbas Kapombe wakienda Ndanda.

Aidha, wachezaji wengine wawili waliokuwemo kwenye orodha hiyo ni Joshua John Thawe, aliyekwenda timu iliyopanda daraja ya Njombe Mji, huku Singida United ikifanikiwa kumtwaa kiungo Mudathir Yahya.

Katika hatua nyingine, bado tunaendelea na mazungumzo na baadhi ya timu ambazo zinamtaka kwa mkopo beki wetu Ismail Gambo, moja ikiwa ya nje ya nchi na zingine za hapa nchini.

Uamuzi wa kuwatoa nyota hao ni sehemu ya mapendekezo ya benchi la ufundi la Azam FC chini ya Kocha Mkuu, Aristica Cioaba, lengo kubwa likiwa ni kuwapa fursa ya kucheza mechi nyingi zaidi ili kujijenga na hatimaye katika siku za usoni kurejea kikosini.

Azam FC imekuwa na utamaduni wa kulinda vipaji vya wachezaji wake kupitia fursa hiyo, itakumbukwa kuwa kwa msimu miwili mfululizo tuliwatoa kwa mkopo wachezaji wetu kiungo Braison Raphael na winga Joseph Kimwaga.

Wachezaji hao wamerejea hivi sasa wakiwa vizuri baada ya kukomaa vilivyo kupitia mechi walizokuwa wakicheza, hivyo tunaamini fursa hiyo itazidi kuwaendeleza wachezaji hao na kuwajenga zaidi huko waendapo.

Kwa habari zaidi katika kipindi hiki cha usajili, tunakuomba uendelee kufuatilia vyanzo vyetu vya habari, mtandao wetu www.azamfc.co.tz , akaunti ya facebook ‘Azam FC’, Instagram ‘azamfcofficial’.