KIPA mpya wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Razak Abalora, kutoka nchini Ghana tayari ameshatua nchini jana usiku, huku akiwa ameanza rasmi mazoezi leo Jumatatu jioni.

Abalora, 20, amesajiliwa na Azam FC akitokea WAFA SC ya Ghana, alikoiongoza timu hiyo kushika nafasi ya pili kwenye ligi hadi sasa huku akiwa na rekodi ya aina yake ya kucheza mechi 12 bila wavu wake kuguswa kati ya 22 alizocheza.

Mbali na kuidakia WAFA, pia Abalora ni kipa tegemeo wa kikosi cha pili cha timu ya Taifa ya Ghana ‘Black Stars’, kinachoshiriki hatua ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), michuano itakayofanyika mwakani nchini Kenya.

Licha ya uchovu wa safari, kipa huyo alijitahidi kuhudhuria mazoezi hayo jambo lililomfurahisha Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba na Kocha wa Makipa, Idd Abubakar.

Ujio wa kipa huyo unaifanya idara ya langoni ya Azam FC kuwa na makipa watatu, wengine wawili wakiwa ni Mwadini Ally na Benedict Haule, huku Metacha Mnata, akitolewa kwa mkopo kwenda Mbao ya mkoani Mwanza.