NYOTA watatu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, waliokuwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, wameanza rasmi mazoezi leo Jumapili jioni wakiungana na wenzao kuendeleza maandalizi ya msimu ujao

Wachezaji hao walioripoti ni nahodha Himid Mao ‘Ninja’, kiungo Salmin Hoza na winga Joseph Mahundi, ambao walikuwa kwenye kampeni ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) mwakani na kutolewa na Rwanda ‘Amavubi’.

Mbali na nyota hao, pia mazoezi hayo yamehudhuriwa kwa mara ya kwanza na wachezaji wengine wa kigeni, beki wa kati Daniel Amoah na kiungo Stephan Kingue, ambao walishindwa kuripoti awali kutokana na kuwa na ruhusa maalum.

Mashambuliaji Shaaban Idd, anayesumbuliwa na majeraha ya misuli ya nyama za paja, tayari ameanza rasmi mazoezi mepesi akiwa chini ya uangalizi wa karibu wa jopo la utabibu la Azam FC.

Kikosi hicho cha mabingwa wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu uliopita, kitaendelea na mazoezi hayo kwa takribani siku saba kabla ya kutoka tena kwenda kucheza mechi nne za kirafiki za maandalizi ya msimu ujao unaotarajia kuanza Agosti 26 mwaka huu.

Bado uongozi wa Azam FC kwa kushirikiana na benchi la ufundi la timu hiyo, unaangalia ni sehemu gani nzuri na yenye utulivu itakayofaa kwa kambi hiyo ya siku 10.

Hiyo itakuwa ni ziara ya tatu ya Azam FC ya maandalizi, ya kwanza ilikuwa ni ile ya nchini Rwanda ilipokwenda kucheza na mabingwa wa Taifa hilo, Rayon Sports na kupoteza kwa mabao 4-2, na Alhamisi iliyopita ilimaliza ziara nyingine ya Nyanda za Juu Kusini.

Katika ziara hiyo ya Nyanda za Juu Kusini, Azam FC ilicheza jumla ya mechi tatu za kirafiki, ikianza kutoka suluhu na Mbeya City, ikafungwa na Njombe Mji mabao 2-0 kabla ya kumaliza kwa kuichapa Lipuli ya Iringa mabao 4-0.