KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inayofuraha kukutaarifu kuwa leo imefanikiwa kunasa saini ya golikipa, Razak Abalora, raia wa Ghana kwa mkataba wa miaka mitatu.

Abalora, 20, anatua Azam FC akitokea timu ya West African Football Academy (WAFA SC), aliyoiongoza kushika nafasi ya pili hadi hivi sasa kwenye Ligi Kuu Ghana wakiwa na pointi 43 huku vinara Aduana Stars waliocheza mechi mbili zaidi yao wakiwa nazo 44.

Meneja Mkuu wa Azam FC, Abdul Mohamed, alisimamia zoezi hilo wakati kipa huyo akisaini mkataba rasmi wa kuitumikia timu hiyo kuanzia msimu ujao hadi mwaka 2020. utakapoitimika.

Ujio wa kipa huyo aliyependekezwa na Kocha Mkuu, Aristica Cioaba, tunaamini kuwa utazidi kuboresha kikosi katika eneo la ulinzi kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaoanza Agosti 26 mwaka huu.

Hadi anaondoka WAFA, Abalora amefanikiwa kudaka jumla ya mechi 22 za msimu na kuwa ndio kipa pekee wa ligi hiyo anayeongoza kutofungwa mabao katika mechi nyingi kuliko yoyote akiwa amefanya hivyo mara 12.

Ubora wake huo akiwa na umri mdogo tu, umemfanya kuitwa katika kikosi cha pili cha timu ya Taifa ya Ghana ‘Black Stars’ kinachoendelea na harakati za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) mwakani nchini Kenya.

Kikosi cha Azam FC hadi hivi sasa kwenye idara hiyo kimesheheni vizuri kikiwa na makipa wengine watatu wazawa, ambao ni mkongwe Mwadini Ally, Benedict Haule, aliyerejea nyumbani akitokea Mbao FC pamoja na kipa anayechipukia, Metacha Mnata aliyepandishwa kutoka timu ya vijana ‘Azam U-20’.

Azam FC inamtakia kila la kheri Abalora katika maisha yake mapya ya soka ndani ya viunga vya Azam Complex, tunaimani ataendeleza rekodi yake nzuri akiwa na uzi huo mpya na hatimaye kufanikisha malengo yaliyowekwa na klabu.