KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Aristica Cioaba, ameweka wazi kuwa ipo siku matokeo mazuri yatawaumbua wale wote wanaoiponda timu hiyo hivi sasa.

Mashabiki wengi wa soka wamekuwa wakiiongelea vibaya timu hiyo kutokana na uwekezaji mpya kwenye kikosi unaofanywa hivi sasa wa kuwapa nafasi wachezaji vijana, wakidai hautaisaidia Azam FC.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu uliopita, wamemaliza ziara ya Nyanda za Juu Kusini jana kwa kishindo baada ya kuilaza Lipuli ya Iringa mabao 4-0.

Akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz Cioaba alisema kuwa ziara hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwenye kikosi chake kutokana na kumsaidia kuwajua wachezaji wake walioko kikosini.

“Leo (jana) niliongea na wachezaji waingie uwanjani na kuongeza umakini, niliwaambia kuwa sitaki tena kuona makosa yaliyojitokeza kwenye mechi mbili zilizopita na timu ikafanikiwa kutimiza hilo na kucheza vizuri na kupata matokeo hayo.

“Lakini inahitaji muda mrefu wa kufanya kazi najua matatizo yaliyoko kwenye kikosi, nitarejea nyumbani (Azam Complex) na kuendelea na mipango yangu ya kufanya mazoezi mazuri, kupata mechi nyingi za kirafiki, wachezaji wote walioko timu ya Taifa kurejea na wengine kuja, na kundi lote kufanya mazoezi ya pamoja ili kuwa na maandalizi mazuri ya kuelekea kwenye ligi,” alisema.

Kuanza na kuingiza mbinu

Cioaba alisema kwa sasa mara baada ya kurejea Dar es Salaam, anatarajia kuanza rasmi mazoezi ya kuipika kiufundi timu hiyo pamoja na kuwapa mbinu wachezaji.

“Baada ya hapo nitachagua timu yangu, na kuweka kichwani kwangu namna gani timu inatakiwa kucheza hapo baadaye, hivi sasa nina muda mzuri wa kuiunganisha timu kwa kuijenga kiufundi na nina uhakika tutafanya vizuri na kila mmoja atajionea namna kikosi chao kitakavyokuwa na wale waliokuwa wanatuponda matokeo yatawaumbua,” alisema.

Huu si wakati wa matokeo

Kocha huyo wa zamani wa Aduana Stars ya Ghana, aliendelea kusisitiza kuwa huu si wakati wa mashabiki wa timu kuangalia matokeo bali ni kipindi cha mwanzo cha kuwajenga wachezaji kupitia mazoezi ya nguvu.

“Narudia tena kuongea kwa wale wanaoelewa mpira wa miguu, hiki ni kipindi cha maandalizi ya msimu ujao na timu inatakiwa kufanya kazi na wachezaji wapya wanakuja na unatakiwa kuangalia uwezo wao, kwa sasa hii si Azam FC kamili, wachezaji wengine wataongezeka wakitoka timu ya Taifa, nina imani baada ya wiki mbili mtaona sura halisi ya kikosi cha Azam,” alisema.

Alisema wachezaji waliopewa mapumziko ya siku saba mara baada ya kutoka timu ya Taifa, wanatarajia kumaliza likizo hiyo ndani ya siku mbili hizi na wataanza mazoezi na wenzao Jumapili ijayo jioni.

“Ni wachezaji muhimu sana, ninao wachezaji wanne au watano wazuri kutoka kwenye kikosi hicho, Shaaban (Idd) na Mbaraka Yusuph wao ni majeruhi, kama kila mchezaji kikosini akiwa fiti na tayari, nina uhakika naweza kuibadilisha Azam FC na kuwa bora zaidi,” alisema.