KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeacha gumzo kubwa kwa wakazi na mashabiki wa soka mkoani Iringa kufuatia kandanda safi waliloonyesha na kuichapa Lipuli mabao 4-0 jana.

Mchezo huo ulikuwa maalum wa kirafiki wa kujiandaa na msimu ujao, na mabao ya Azam FC yamefungwa na Yakubu Mohammed, Wazir Junior, Yahya Zayd na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Mamia ya mashabiki wa soka mkoani humo walishindwa kujizuia kuonyesha hisia zao kwa timu hiyo, baada ya kuvamia uwanjani mpira ulipomalizika na kuanza kujichanganya na wachezaji wa timu hiyo ili kupiga nao picha na wengine wakienda mbali zaidi na kuwapongeza kwa namna walivyocheza.

Hilo halikuwapa shida wachezaji wa Azam FC, ambao walijichanganya nao na kukubali kupiga nao picha kila walipoombwa kufanya hivyo.

Mara baada ya wachezaji wote kuingia kwenye basi, mashabiki waliiaga Azam FC kwa kuanza kulipungia mikono ya kwaheri lilipokuwa likiondoka huku wengine wakilikimbiza na asilimia kubwa wakipiga makofi.

Katika kuonyesha wanawajali, nao waliwapungia mikono ya kwaheri jambo ambalo liliendelea kufurahiwa na mashabiki wao.

Tokea Azam FC iwasili mkoani hapa kwa ajili ya mchezo huo, imekuwa ikkivuta mashabiki wengi kuanzia kwenye siku ya kwanza mazoezini hadi jana katika mechi, jambo ambalo linadhihirisha kuwa walikuwa ‘wameimiss’ burudani ya soka ya VPL siku nyingi.