KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, jioni hii imemaliza ziara yake Nyanda za Juu Kusini kwa kuichapa Lipuli ya Iringa mabao 4-0, katika mchezo wa kirafiki wa maandalizi ya msimu ujao uliofanyika Uwanja wa Samora mkoani humo.

Shukrani kwa mabao safi yaliyofungwa na beki Yakubu Mohammed, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ huku Wazir Junior na Yahya Zayd nao wakiifungia kwa mara ya kwanza timu hiyo.

Azam FC ikiwa kwenye mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, imefanikiwa kucheza mechi tatu, ikitoka suluhu na Mbeya City, ikapoteza 2-0 walipocheza na Njombe Mji kabla ya leo kushusha kipigo kikali.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Aristica Cioaba, alikuwa haangalii matokeo yoyote katika ziara hiyo, bali alijiwekea malengo ya kukiangalia kikosi chake chote kwa kuwapa nafasi ya kucheza wachezaji wote.

Mchezo huo ulianza kwa kasi kubwa, timu zote zikishambuliana kwa zamu, lakini walikuwa ni Azam FC walioweza kuandika bao la uongozi dakika ya 26, lilowekwa kimiani na Yakubu aliyeitumia vema kona safi iliyochongwa na Enock Atta.

Mshambuliaji mpya wa Azam FC, Wazir Junior, aliyesajiliwa akitokea Toto Africans, aliifungia bao la pili timu hiyo dakika ya 36 na kufungua akaunti ya mabao tokea ajiunge na timu hiyo, akitupia kwa shuti baada ya pasi safi ya kukata pembeni iliyopigwa na Yahaya Mohammed.

Junior alishindwa kuwafurahisha tena mashabiki wa Azam FC, baada ya kukosa bao la wazi dakika ya 45 kufuatia kuukosa mpira wakati akiwa kwenye harakati za kuupiga kabla ya kipa kuudaka vema.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Azam FC iliondoka kifua mbele kwa mabao hayo, ambapo ilikianza kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko akitoka Yahaya na beki David Mwantika na kuingia Yahya Zayd na beki wa kulia Saleh Abdallah.

Yahya alitumia vema nafasi hiyo ndani ya dakika tano tu, kwa kuipatia bao la tatu Azam FC baada ya kumhadaa beki wa Lipuli na kuingia ndani ya eneo la hatari kisha akapiga shuti la chini la kiufundi lililomshinda kipa.

Sure Boy alihitimisha ushindi huo mnono wa Azam FC kwa kuifungia bao la nne timu hiyo dakika ya 60 kwa shuti baada ya kuitumia vema kazi iliyofanywa na kiungo Braison Raphael, aliyekuwa kwenye kiwango bora katika mchezo huo.

Mara baada ya mtanange huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam kesho Alhamisi alfajiri.

Kikosi hicho kitapumzika kwa siku mbili Ijumaa na Jumamosi, kabla ya Jumapili kuendelea na programu ya mazoezi ya kumalizia maandalizi ya msimu ujao.

Kikosi Azam FC leo:

Mwadini Ally, David Mwantika/Saleh Abdallah dk 46, Bruce Kangwa, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Frank Domayo/Masoud Abdallah dk 79, Braison Raphael, Salum Abubakar/Ramadhan Mohammed dk 88, Yahaya Mohammed/Yahya Zayd dk 46, Wazir Junior/Joeph Kimwaga dk 72, Enock Atta/Idd Kipagwile dk 61