KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, jioni hii imecheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Njombe Mji kujiandaa na msimu ujao na kupoteza kwa mabao 2-0.

Huo ni mchezo wa pili wa kirafiki wa Azam FC kwenye ziara yake ya Nyanda za Juu Kusini kujiandaa na msimu ujao, ambapo ilitoka suluhu katika mchezo wa kwanza dhidi ya Mbeya City.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, alibadilisha kikosi chote kilichocheza mchezo wa kwanza isipokuwa beki David Mwantika, ambapo kilichosheheni wachezaji wengi wapya vijana.

Kocha huyo alikibadili tena kikosi hicho dakika ya 51 wakati kilipomaliza kipindi cha kwanza kwa kuruhusu wavu wake kuguswa mara moja, bao lilofungwa na Adam Baiko dakika ya 34.

Njombe Mji ikajipatia bao la pili dakika ya 80 lililofungwa na Rafael Siame.

Tayari Cioaba ameweka wazi kutoangalia matokeo zaidi katika mechi zake hizi za kirafiki, ambapo amedai kwa sasa amepanga kukisoma kikosi chake kwa kuwapa nafasi ya kucheza wachezaji wake wote na kujua ni kikosi gani kitamfaa kwa msimu ujao.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi hicho kitaanza tena safari ya kuelekea mkoani Iringa kesho saa 3.00 asubuhi kwa ajili ya kwenda kucheza mtanange wa mwisho wa kirafiki dhidi ya Lipuli ya huko, utakaofanyika Uwanja wa Samora Julai 26 mwaka huu.

Kikosi cha Azam FC leo:

Metacha Mnata, Saleh Abdallah/Ismail Gambo dk 51, Abdul Omary/Bruce Kangwa dk 51, David Mwantika/Aggrey Morris dk 51, Abdallah Kheri/Yakubu Mohammed dk 51, Abbas Kapombe/Frank Domayo dk 51, Masoud Abdallah/Bryson Raphael dk 51, Stanslaus Ladislaus/Salum Abubakar dk 51, Yahya Zayd/Wazir Junior, Mudathir Yahya/Yahaya Mohammed dk 51, Joseph Kimwaga/Enock Atta dk 51