KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, tayari imewasili Makambako, mkoani Njombe leo mchana ikitokea Mbeya huku jambo la kuvutia zaidi timu hiyo imeteka mashabiki wa mjini katika mazoezi yaliyofanyika jioni hii.

Azam FC imewasili mkoani humo tayari kabisa kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ngeni iliyopanda daraja Njombe Mji, utakaofanyika Uwanja wa Amani, Makambako kesho Jumatatu saa 10.30 jioni.

Huo utakuwa ni mchezo wake wa pili wa maandalizi ya msimu ujao baada ya ule wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Sokoine, Mbeya jana dhidi ya Mbeya City ulioisha kwa suluhu

Kikosi hicho mara baada ya kuwasili, jioni hii kilifanya mazoezi yaliyowateka mashabiki wengi waliohudhuria kuwaona nyota wa Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup), ambao muda mwingi walionekana kuwafurahia wakati wakiwa mazoezini.

Jambo jingine walilokuwa wakishangaa ni basi kubwa la kisasa linalotumiwa na timu hiyo, ambalo kwa sasa limeteka Afrika Mashariki kutokana na timu nyingi kutokuwa na basi la aina hiyo.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Aristica Cioaba, mara baada ya mazoezi hayo ameuambia mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa anatarajia kukifanyia marekebisho kikosi chake katika mchezo huo wa kesho ikiwa ni sehemu ya kuwapa nafasi ya kucheza wachezaji wote kikosini.

“Jana tulicheza mchezo wetu wa kwanza dhidi ya Mbeya City, ni mchezo uliokuwa mzuri timu yangu ilitengeneza takribani nafasi nne za kufunga kuliko wapinzani wetu (Mbeya City) lakini hawakuweza kuzitumia.

“Nilikuwa siangalii matokeo bali nilikuwa nawaangalia kiufundi zaidi wachezaji wangu, hatuna muda mrefu sana tokea tuanze maandalizi yetu, timu kwa sasa ina ufiti asilimia 50 kwani bado tupo kwenye programu ya mazoezi ya kujenga nguvu, ufundi na mbinu kidogo,” alisema.

Kocha huyo raia wa Romania alisema kuwa muda mrefu ataanza kuwapika ipasavyo kwenye mazoezi ya mbinu na ufundi zaidi, ili kuiunganisha vema timu kwa ajili ya changamoto ya kupambana katika mechi zake msimu ujao.

“Mashabiki wa Azam FC wasiwe na wasiwasi, hii ni timu yao sapoti yao kubwa inahitajika msimu ujao, na mimi naamini muda si mrefu timu hii itakuwa ni timu bora sana hapa Tanzania na Afrika, mpira ni mchezo wa kuhitaji muda na uvumilivu, nawashukuru sana viongozi na mabosi wangu kwa sapoti wanayoendelea kunipa,” alisema.

Mara baada ya Azam FC kumalizia changamoto hiyo ya mchezo wa pili, itaelekea tena mkoani Iringa Julai 25, kwa ajili ya kwenda kucheza mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya Lipuli ya huko, utakaofanyika Julai 26 kwatika Uwanja wa Samora.