KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kesho Jumamosi inatarajia kushuka dimbani kupambana na Mbeya City katika mchezo wa kirafiki wa maandalizi ya msimu ujao.

Tayari kikosi hicho kimeshawasili mjini Mbeya saa 4.00 usiku jana kikiwa na msafara wa wachezaji 26, kwa ajili ya mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Sokoine, mjini humo.

Mara baada ya mchezo huo, Julai 23 mwaka huu kikosi hicho kitaelekea mkoani Njombe, kukipiga na Njombe Mji mtanange utakaofanyika Uwanja wa Makambako Julai 24 kabla ya kuelekea mkoani Iringa kucheza na Lipuli Julai 26 katika Uwanja wa Samora mjini humo.

Akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, alisema atazitumia mechi hizo zote kama sehemu ya kukisoma kikosi chake kwa kuwaangalia namna wanavyopambana katika mechi hizo kulingana na mifumo yake.

“Siko hapa kuangalia matokeo zaidi kwenye mechi hizi, huu ni wakati wa kuijenga timu, natarajia kuwapa nafasi wachezaji wote kikosini, baada ya mechi hizi nitajua wachezaji gani wa kujumuika nao msimu ujao,” alisema.

Alisema mashabiki wanatakiwa kuendelea kuisapoti timu hiyo, wachezaji pamoja na uwekezaji unaoendelea kufanyika, na kudai kuwa hapo baadaye wataanza kuona faida ya mikakati inayoendelea kufanyika.

Katika hatua nyingine, alithibitisha kurejea kwa kiungo nyota Mcameroon, Stephan Kingue, aliyewasili jijini Dar es Salaam leo na kudai kuwa pia kesho wanatarajia kumpokea beki Daniel Amoah, ambao wote wawili wataungana na timu itakaporejea jijini Dar es Salaam Julai 27 mwaka huu.

Mara baada ya kurejea Dar es Salaam, kikosi hicho kitapumzika siku mbili kabla ya kurejea mazoezini Julai 30.