KIPA mpya wa Azam FC, Benedict Haule, anaamini ya kuwa kujituma, kutokata tamaa, kuwatii makocha na viongozi, ndio vitu muhimu vilivyombeba mpaka kufikia kiwango alichonacho na kurejea kwenye timu hiyo.

Haule aliyechezea kikosi cha Mbao msimu uliopita, amerejea tena Azam FC kwenye kipindi hiki cha usajili, timu aliyoikacha miaka mitatu iliyopita akiwa kwenye academy ya timu hiyo na kujiunga na Panone ya mkoani Kilimanjaro. 

Akifanya mahojiano maalumu na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz Haule alisema jambo la kwanza alilokuwa akijiamini tokea mwanzo ni yeye kuwa na uwezo wa kucheza soka na kuamini ipo siku moja kipaji chake hicho kitamtoa.

“Sikukata tamaa baada ya kutoka hapa (Azam FC), nikaamini kuwa nitajituma zaidi ya hapa kwa kuonyesha kiwango changu, kwamba nilipotoka hapa na kwenda Panone nilienda na kuonyesha jitihada na tukaweza kuipandisha timu hadi Ligi Daraja la Kwanza, nikaondoka nikaenda Coastal (Union) na huko tukaipambania timu na baada ya hapo nikaenda Mbao FC kabla ya kurejea hapa,” alisema.

Afurahia kurejea Azam Complex

Kipa huyo alisema kuwa anafurahia kurejea tena Azam FC huku akidai kuwa hilo linampa faraja ya kuweza kuongeza jitihada zake ili aweze kufanya vizuri katika kikosi hicho na hatimaye kuitwa kwenye timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

“Nimefarijika sana kwa sababu nimerudi tena nyumbani sehemu ambayo nilikuwepo, ni kitu ambacho kilinifariji sana ili nizidi kuongeza jitihada na naamini mbeleni yapo mazuri zaidi ya haya, kwa hiyo ni jitihada tu nitazidi kuongeza ili niweze kufika mbali zaidi,” alisema.

Ni mapambano tu

Alisema kuwa jambo kubwa litakalomfanya kufikia mafanikio na kuisaidia timu hiyo ni kuhakikisha anapambana huku akidai ataonyesha kiwango kikubwa tofauti na kile kinachofahamika.

“Kipya ni mapambano tu, ni kupambana zaidi ya nyuma nilivyokuwa nafanya kuongeza jitihada na kujituma zaidi ya hapa, naamini nitaonyesha kiwango kikubwa zaidi ya nilichoonyesha huko nyuma,” alisema.

Kugombea namba

“Mpira ni mchezo wa nafasi na wa kujituma, naamini ukijituma kocha anaona, benchi la ufundi linaona kwa hiyo nafasi inakuwepo unacheza na unaonyesha kile ulichokuwa nacho,” alisema kipa huyo mwenye umbo kubwa aliyeisadia sana Mbao kufika fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) msimu uliopita.

Azam FC itafika mbali

Haule aliyekabidhiwa jezi nambari 30, anaamini ya kuwa kujitambua na kujituma uwanjani kwa wachezaji wote kikosini kutaifanya Azam FC kufika mbali msimu ujao.

“Cha kwanza ni kujitambua na kujituma, kwamba kujua sasa hivi ni wakati gani na timu inahitaji nini ukipewa nafasi uonyeshe jitihada zako, mazoezini kujituma mwenyewe, kuonyesha umakini kwenye mechi, naamini timu tutaipeleka mbali, tutafika mbali,” alisema.

Kauli kwa mashabiki

Kipa huyo aliwatoa hofu mashabiki wa Azam FC kwa kuwaambia kuwa msimu ujao watapambana vilivyo ili kuifikisha timu hiyo pazuri.

“Mashabiki watarajie mazuri zaidi, tutajitahidi kwa nguvu zote, tutajitahidi kwa uwezo wetu wote, tutajituma tuhakikishe timu tunaifikisha pazuri, kushika nafasi ya kwanza au ya pili, naamini tutafanya kazi na timu tutaifikisha pazuri,” alisema.

Haule anatarajia kukabiliana na upinzani mkubwa kikosini kutoka kwa kipa mzoefu, Mwadini Ally na kinda anayekuja kwa kasi, Metacha Mnata, ambaye ametokea kwenye academy ya timu hiyo.