TIMU ya vijana chini ya umri wa miaka 13 ya Azam FC (Azam U-13) imezidi kufanya kweli kwenye Ligi ya Vijana ya Azam (Azam Youth League U-13) baada ya kuichapa Rendis Academy mabao 2-1 katika muendelezo wa michuano hiyo leo.

Huo ni ushindi wa pili mfululizo baada ya kutoka kufungwa mabao 3-0 na Bom Bom SC wiki tatu zilizopita kabla ya kuichapa Ilala Academy 2-0 wikiendi iliyopita.

Michuano hiyo iliyoanza kutimua vumbi Mei 26 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, imefikisha wiki ya saba hivi sasa ikishirikisha timu sita, zingine zikiwa ni Magnet Youth Academy na JMK Park Academy.

Mechi nyingine zilizopigwa leo, ilishuhudiwa JMK ikiichapa Magnet mabao 4-1 huku Bom Bom ikiendeleza wimbi la ushindi wa asilimia 100 kwenye michuano hiyo kwa kuilaza Ilala 3-0.

Michuano hiyo itaendelea tena, wikiendi ijayo Julai 22, kwa mechi tatu, Rendis itaanza kukipiga na Bom Bom saa 3.00 asubuhi, wenyeji Azam FC watachuana na Magnet huku mchezo wa mwisho ukiwahusisha Ilala na JMK.