BENCHI la Utabibu la Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, limetoa ripoti ya majeraha ya washambuliaji Shaaban Idd na Mbaraka Yusuph, inayoeleza kuwa wanatakiwa kukaa nje ya dimba kwa muda wiki tatu zijazo.

Wachezaji hao waliokuwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, kilichokuwa kikishiriki michuano ya COSAFA nchini Afrika Kusini iliyomalizika hivi karibuni.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa, alisema kuwa wachezaji wote hao wawili walifanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Muelmed, iliyopo mjini Pretoria, Afrika Kusini.

Daktari huyo bingwa wa tiba za michezo na za kawaida, aliyewachukua timu ya Taifa na kuwapeleka kwenye hospitali hiyo kufanyiwa vipimo alisema kuwa Idd anasumbuliwa na matatizo ya misuli ya paja, akidai kwa mujibu wa vipimo amechanika misuli miwili ya eneo hilo.

“Kwa hiyo Shaaban Idd alipatiwa matibabu katika Hospitali hiyo ya katika Hospitali ya Muelmed na atatakiwa kupumzika kwa muda wa wiki tatu na baada ya hapo ataanza mazoezi madogo madogo na kuweza kurejea kwenye ushindani,” alisema.

Akizungumzia tatizo linalomkabili Yusuph, daktari huyo alisema kuwa hali ya ubaridi nchini Afrika Kusini ilipelekea kupata Henia.

“Katika sehemu fulani ya hiyo Henia kulikuwa na ukosefu wa damu au kwa kitaalamu tunaita ‘Strangulation’, kwa hiyo ilibidi afanyiwe operesheni na baada ya kufanyiwa operesheni alikaa hospitali siku nne kabla ya kurejea nchini.

“Na yeye (Yusuph) kwa mujibu wa programu yake katika wiki hizi mbili za kwanza anatakiwa kupumzika na baada ya wiki moja kupita yaani ikiwa ni wiki ya tatu atatakiwa kurejea uwanjani kucheza na wenzie kama kawaida,” alisema.

Alisema kuwa kwa sasa wachezaji wengine wako vizuri wakiendelea na mazoezi ya kujiandaa na msimu ujao, yaliyoanza wiki chache zilizopita.