KOCHA Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, anaamini kuwa Rais mpya ajaye wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ataipa nafasi timu hiyo kuutumia uwanja wake wa nyumbani wa Azam Complex katika mechi za nyumbani dhidi ya Simba na Yanga.

Tangu Klabu hiyo Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati ianze kuutumia uwanja wake huo, imekuwa ikinyimwa fursa na TFF kuutumia uwanja wake huo wa nyumbani pindi inapocheza na Simba na Yanga, ambapo imekuwa ikizichezea Uwanja wa Taifa au ule wa Uhuru.

TFF ambayo ipo kwenye mchakato wa uchaguzi hivi sasa utakaofanyika Agosti 12 mwaka huu, imekuwa haina sababu zenye mashiko za kuzipeleka mechi hizo nje ya Azam Complex, ambapo imekuwa likieleza sababu za kiusalama kuzuia, kazi ambayo Jeshi la Polisi Tanzania halijawahi kukiri kuishindwa.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu uliopita wamekuwa wakinufaika na mechi zingine, zikiwemo zile zinazoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ambalo limekuwa likiiruhusu Azam FC kuutumia uwanja wake huo katika mechi zao za kimataifa kutokana na kukidhi viwango vyote vya usalama vinavyotakiwa.

Akifanya mahojiano maalumu na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz Cioaba alisema anaamini Rais huyo ataweka usawa kwenye soka la Tanzania kwa timu inayostahili kushinda kupata matokeo hayo bila kuweka upendeleo kwa baadhi ya timu.

“Naamini huu mwaka kutakuwa na haki kwenye soka, na nafasi kwa timu zote ile inayocheza soka zuri kupata matokeo na hii inaweza kutupa nafasi ya kukaa kileleni na kuchukua ubingwa, kama ninao uwanja wangu huu wa nyumbani (Azam Complex), naiomba TFF ielewe ya kuwa kama mimi natoka kwenda kucheza ugenini basi na wao nataka waje kucheza hapa kwenye uwanja wangu wa nyumbani.

“Sio kama msimu uliopita mimi kama nataka kucheza na Simba, mechi zote mbili nacheza Uwanja wa Taifa nyumbani kwa Simba na mechi za Yanga hivyo hivyo, naamini Rais mpya wa TFF atabadilisha hili na mechi hizo za nyumbani dhidi ya Simba na Yanga kupigwa hapa na mambo yote yatakuwa na haki na timu zote kuwa nafasi ya kushinda taji,” alisema.

Alisema ameiona ratiba ya ligi hiyo kuwa ataanzia mechi ugenini dhidi ya Ndanda (Agosti 26) kabla ya mechi ya pili kucheza na Simba na kudai ni ratiba nzuri na kwa sasa anakipanga kikosi chake kuweza kufanya vizuri.

“Tumeanza maandalizi ya msimu mpya, kitu cha kwanza ninachopenda kuwaambia mashabiki wa Azam FC, nimeona wanazungumza sana kuhusu kuondoka kwa wachezaji wanne waliokuwa bora hapa na kwenda kwenye timu nyingine, lakini wanatakiwa kuelewa kuwa huu ni mpira na hii ni mipango ya timu.

“Najua Aishi (Manula) ni kipa mzuri na amecheza hapa vizuri sana akianzia kwenye academy, pia Bocco (John) ni mchezaji wa muda mrefu hapa amekaa miaka saba hadi nane na kufanya makubwa, naye pia ameenda kwenye timu nyingine, mchezaji mwingine ni Kapombe (Shomari) ameondoka, huu ni mpira mashabiki wanatakiwa kuelewa hii haitokei kwa Azam FC tu, wacheza wanaondoka na wengine hurejea unaona kila nchi katika kipindi hiki cha maandalizi mchezaji mzuri anaenda kwenye timu nyingine na mwingine anakuja.

“Huu ni mpango wa baadaye wa Azam FC, mashabiki wanatakiwa kutuamini na kuiamini timu, na nina uhakika Azam FC haiwezi kwenda chini, ninaamini Azam FC itakuwa juu msimu ujao,” alisema.

Kuhusu wachezaji wapya

Akizungumzia wachezaji wapya, kocha huyo wa zamani wa Aduana Stars ya Ghana alisema: “Wamekuja wachezaji wapya wadogo, ambao ni wazuri sana kwa hapa Tanzania, mimi niliwaona hapa kwenye ligi na nikapendekeza wasajiliwe hapa na ninaona kakwa ushauri wangu ni wachezaji bora sana kwa ajili ya baadaye.”

Alisema Azam FC ni klabu iliyojipanga vizuri, huku akiwaondoa hofu mashabiki kutowawazia wachezaji walioondoka, na kudokeza kuwa anatarajia kuwafanyia sapraizi kwa kushusha wachezaji wawili wa kiwango cha juu kutoka nje ya nchi.

“Bado tuna wachezaji wazoefu kwenye timu, ambao wamecheza msimu uliopita Morris (Aggrey) yupo, Yakubu yupo, Bruce (Kangwa) yupo, Himid (Mao) yupo, Domayo (Frank) yupo, Daniel (Amoah) yupo, Sure Boy (Salum Abubakar) bado yupo na wachezaji kutoka academy niliowapa nafasi msimu uliopita kama Masoud (Abdallah), Shaaban (Idd) wote hapo, nadhani nina baadhi ya wachezaji wazoefu na baadhi wachanga.

“Wote watakaa pamoja kwenye kazi, na hapo baadaye tutakuwa na timu bora, huu ni ujumbe wangu kwa mashabiki wa Azam FC wanaoipenda Azam FC, kwa wafanyakazi, kwa wachezaji na kwa mtu yoyote anayeipenda Azam FC waipende Azam FC na kama wakiipenda kweli kiwango cha timu kitakwenda juu,” alisema.

Cioaba alisema anaushukuru uongozi wa timu hiyo kwa kuifanyia kazi ripoti yake aliyoiwasilisha kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao, akisema mbali na kuwa na kambi ya siku nje ya Dar es Salaam wakienda kucheza mechi za kirafiki Nyanda za Juu Kusini, pia uongozi wa timu hiyo unaendelea kufanyia kazi uwezekano wa kuweka kambi ya siku 10 nchini Kenya au Uganda mwezi ujao kabla ya kuanza kwa ligi.