MARA baada ya kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kuwasili jijini Dar es Salaam jana usiku kikitokea nchini Rwanda, wachezaji wamepewa mapumziko ya siku moja kwa ajili kuondoa uchovu kabla ya kesho Jumatano kuendelea na maandalizi ya msimu mpya 2017-18.

Kikosi hicho kilikwenda jijini Kigali nchini humo kwa ajili ya kwenda kusherehesha ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo (Azam Rwanda Premier League) walioutwaa Rayon Sports kwa kucheza nao mechi maalumu ya kirafiki walipokuwa wakikabidhiwa taji hilo Jumamosi iliyopita na kupoteza kwa mabao 4-2.

Mapumziko hayo hayawahusu wachezaji ambao hawakuwemo kwenye safari hiyo, ambao ni mabeki Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, winga Enock Atta Agyei na mshambuliaji Wazir Junior.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, ameshatua nchini jana Jumatatu, na leo Jumanne ataanza mazoezi pamoja na wachezaji hao ambao hawakuwepo kwenye ziara hiyo.

Wachezaji wote waliotoka kwenye safari hiyo watatakiwa kuendelea na mazoezi kesho jioni wakiungana na wenzao chini ya Kocha Cioaba, isipokuwa Mbaraka Yusuph na Shaaban Idd, ambao ni wagonjwa na hivi sasa wakiendelea na matibabu.

Ni wachezaji watatu tu ambao bado hawajaripoti, ambao ni Waghana Daniel Amoah, mshambuliaji Samuel Afful na kiungo Mcameroon Stephan Kingue, ambao muda wowote kuanzia sasa watajiunga na wenzao.

Nahodha Msaidizi, Himid Mao ‘Ninja’, kiungo mpya Salmin Hoza, beki wa kushoto Gardiel Michael na winga Joseph Mahundi aliyeongezwa jana, wenyewe hawamo kikosini kutokana na kuwa kwenye majukumu ya timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

Wachezaji hao wapo Stars, inayoendelea na maandalizi kujiandaa na mchezo wa kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) dhidi ya Rwanda ‘Amavubi’ utakaofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Jumamosi ijayo.