KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeahidi kuonyesha soka safi kwa mashabiki wa soka nchini Rwanda kuelekea mchezo wa kesho Jumamosi dhidi Rayon Sports, utakaofanyika Uwanja wa Nyamirambo, Kigali saa 10.30 jioni.

Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa timu hiyo, Phillip Alando, kwenye mkutano maalum wa waandishi wa habari uliofanyika muda mchache uliopita kwenye Makao Makuu ya Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA).

“Tunawashukuru sana wenzetu Rayon Sports kwa nafasi waliyotupa kucheza nao, wangeweza kuchagua timu nyingine lakini wametuchagua sisi ni jambo zuri, tunachoahidi ni soka safi kesho kwa mashabiki.

“Najua wenzetu wamejipanga kuwa na furaha mara mbili kesho, moja watakapokuwa wakikabidhiwa kombe na nyingine wakitaka kupata ushindi, lakini sisi tumejipanga kuwapa machungu kwa kuwafunga,” alisema.

Alando alisema Azam FC imewasili ikiwa na wachezaji 22, wakiwemo wachezaji vijana sita waliopandishwa timu kubwa na wachezaji wawili wa kimataifa, beki wa kushoto Bruce Kangwa na mshambuliaji Yahaya Mohammed.

Kwa upande wake, Rais wa Rayon Sports, Gacinya Chance Denis, alisema wameamua kuichagua Azam FC kutokana na ukubwa wa timu hiyo huku akisema ndio timu bora Afrika Mashariki na Kati kwa ubingwa wa Kagame Cup walioutwaa.

Mchezo huo ambao pia utarushwa na Azam TV kupitia chaneli yake ya Azam TWO, utakuwa ni mahususi kwa Rayon Sports kusheherekea ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Rwanda walioutwaa, ambapo watakabidhiwa rasmi kombe lao na FERWAFA.