KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kuondoka nchini kesho Jumatano alfajiri, tayari kabisa kuelekea Rwanda kukipiga na Rayon Sports Jumamosi ijayo.

Kikosi cha Azam FC hivi sasa kipo kwenye maandalizi makali kujiandaa na msimu ujao, ambapo itacheza na Rayon katika mchezo maalum wa kusherehesha ubingwa wa Ligi Kuu Rwanda iliyoutwaa timu hiyo.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi hicho kitaanza safari ya kurejea nchini Jumapili ijayo.

Mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi na Ngao ya Jamii msimu uliopita, wanaendelea na mazoezi huku ikiwakosa wachezaji wake kadhaa Nahodha Msaidizi Himid Mao ‘Ninja’, beki Erasto Nyoni, kiungo Salmin Hoza na washambuliaji Mbaraka Yusuph na Shaaban Idd, ambao wako timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

Nyota hao wako na Stars inayoshiriki michuano ya Kombe la COSAFA inayoendelea nchini Afrika Kusini, ambapo timu hiyo ikiwa imetinga hatua ya nusu fainali na ikitarajiwa kucheza na Zambia kesho.

Wengine ambao bado hawajawasili ni mabeki Yakubu Mohammed, Daniel Amoah, winga Eneock Atta Agyei (Ghana), kiungo Mcameroon Stephan Kingue na mshambuliaji Wazir Junior, aliyesajiliwa akitokea Toto Africans ya Mwanza.