LIGI ya Vijana chini ya umri wa miaka 13 ya Azam (Azam Youth League U-13) imemaliza mzunguko wa kwanza leo asubuhi kwa timu zote sita kushuka dimbani ndani ya viunga vya Azam Complex, Chamazi.

Ligi hiyo iliyoanza kutimua vumbi Mei 27 mwaka huu, ilishuhudiwa wenyeji Azam FC U-13 wakimaliza raundi hiyo kwa kupoteza 3-0 dhidi ya vinara wa michuano hiyo, Bom Bom SC.

Magnet Youth nayo iliichapa Ilala Academy mabao 2-1, huku mtanange wa mwisho ukimalizika kwa JMK Park Academy kutoka suluhu na Rendis Academy.

Akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo huo, Mkuu wa Maendeleo ya Soka la Vijana la Azam FC, Tom Legg, alionyesha kufurahishwa sana na kiwango walichoonyesha vijana wake katika mchezo huyo licha ya kupoteza.

“Matokeo hayakuakisi mchezo ulivyokuwa, tumefanikiwa kucheza vema na kumiliki mchezo kwa asilimia kubwa na kutengeneza nafasi saba za wazi, lakini hatukuweza kuzitumia vema kwa kufunga mabao, Bom Bom wametengeneza nafasi chache na wameweza kuzitumia.

“Lengo la michuano hii si kuangalia matokeo bali ni kuangalia uwezo wa wachezaji, kiufundi katika umri huu mambo makubwa ya kuangalia ni namna gani wachezaji wanaweza kukabiliana na presha ya mchezo pamoja na kuwapa uhuru wa kucheza ili kuwajenga kiuwezo,” alisema Legg.

Hadi raundi ya kwanza inamalizika, vinara wa ligi hiyo ni Bom Bom wakiwa wameshinda mechi zote tano na kujikusanyia jumla ya pointi 15, Azam U-13 inafuatia ikiwa nazo saba, sawa na JMK Park, Rendis imejizolea pointi sita kwenye nafasi ya nne, Ilala Academy ipo nafasi ya tano kwa pointi zake nne huku Magnet Youth ikifunga dimba kufuatia kujisanyia pointi tatu.

Mzunguko wa pili wa michuano hiyo utaanza Jumamosi ijayo (Julai 8) kwenye uwanja huo, kwa JMK Park kumenyana na Bom Bom, Azam kukipiga na Ilala Academy huku Rendis wakichuana na Magnet Youth.