NAHODHA Msaidizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’, amefanikiwa kuwa Mchezaji Bora wa mashabiki wa timu hiyo msimu uliopita.

Ninja ameibuka kidedea baada ya kupigiwa kura nyingi na mashabiki kwenye mitandao ya kijamii ya mabingwa hao (facebook – Azam FC na instagram – azamfcofficial), akiwazidi nyota wengine wawili wa timu hiyo, beki kisiki Yakubu Mohammed na mshambuliaji anayekuja kwa kasi, Shaaban Idd.

Kwa mujibu wa takwimu za mchuano huo, kura zote zilizofanya uamuzi huo kwa kukubaliwa zilikuwa 293, huku ikishuhudiwa Ninja aliyekuwa kwenye kiwango bora kabisa msimu uliopita akizoa zaidi ya nusu ya kura hizo ambazo ni 151.

Mohammed amefuatia katika nafasi ya pili kwa kuvuna jumla ya kura 72 akimzidi kura mbili tu Shaaban aliyefunga dimba baada ya kujikusanyia 70.

Mchakato wa kuwapata wachezaji hao watatu walioingia kwenye kinyang’anyiro hicho uliwahusisha mashabiki katika kurasa hizo za Azam FC ndani ya mitandao hiyo ya kijamii, ambao waliwachagua kwa wingi kuwa wachezaji wa msimu wa timu hiyo.

Ninja ambaye hivi sasa ni Nahodha Msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, amerithi mikoba ya aliyekuwa beki wa timu hiyo, Shomari Kapombe, aliyeitwaa mwaka jana mara baada ya kumalizika kwa msimu wa 2015-2016.