KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo inapenda kuwajulisha wapenzi wa soka nchini kuwa leo imekamilisha usajili wa aliyekuwa kipa wa Mbao, Benedict Haule.

Haule amesaini mkataba wa miaka miwili leo jioni mbele ya Meneja Mkuu wa Azam FC, Abdul Mohamed sambamba na Meneja wa timu, Phillip Alando, utakaoanza kufanya kazi kuanzia Julai Mosi mwaka huu.

Usajili huo unamfanya kipa huyo kurejea tena nyumbani ndani ya viunga vya Azam Complex, kwani aliwahi kulelewa katika kituo cha Azam Academy chini ya Kocha wa Makipa wa Azam FC, Idd Abubakar.

Kipa huyo anaungana na makipa wengine wa Azam FC, Aishi Manula, Mwadini Ally na Metecha Mnata, tayari kabisa kuanza mchakamchaka wa kujiandaa na msimu ujao kuanzia Julai 3 mwaka huu.

Huo ni usajili wa nne kwa Azam FC kuelekea msimu ujao 2017/2018, wengine ambao tayari saini zao zimenaswa ni kiungo nyota Salmin Hoza na washambuliaji wanaokuja kwa kasi Mbaraka Yusuph na Wazir Junior.

Mbali na usajili wa wachezaji hao, tayari benchi la ufundi la mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi na Ngao ya Jamii chini ya Mromania Aristica Cioaba, limefanya uamuzi wa kuwapandisha vijana sita kutoka kituo cha Azam Academy.

Mabeki Abbas Kapombe, Abdul Omary, Godfrey Elias na Ramadhan Mohammed, anayemudu kucheza namba nyingi uwanjani, kiungo Stanslaus Ladislaus na mshambuliaji Yahaya Zaid, aliyeibuka mfungaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza msimu uliopita kwa mabao yake tisa wakati alipokuwa akiichezea kwa mkopo Ashanti United.

Kwa taarifa zaidi za kina, kuhusiana na habari mbalimbali za Azam FC kuelekea kipindi hiki cha usajili, unaombwa kuendelea kufuatilia vyanzo vya rasmi vya habari vya timu hiyo kwenye mtandao wa kijamii wa facebook ‘Azam FC’, instagram ‘azamfcofficial’ na tovuti ya ‘www.azamfc.co.tz’.