KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inayofuraha kubwa kuwataarifu wapenzi wa soka nchini kuwa imefanikiwa kunasa saini za wachezaji wawili wanaokuja kwa kasi, mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Mbaraka Yusuph na kiungo Salmin Hoza.

Usajili huo ni sehemu ya mkakati wa kuboresha kikosi cha timu hiyo kwa kusajili wachezaji vijana wenye vipaji na kuongeza wengine kutoka kwenye kituo chake cha kulea na kukuza vipaji cha Azam Academy.

Nyota hao kwa pamoja kila mmoja amesaini mkataba wa miaka miwili itakayoanza Julai Mosi mwaka huu, na wanafanya ifikie idadi ya wachezaji watatu wapya waliosajiliwa na Azam FC kuelekea msimu ujao 2017-18, mwingine akiwa ni mshambuliaji wa zamani wa Toto African ya Mwanza, Wazir Junior.

Mbaraka aliyetwaa Tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi msimu uliopita, anajiunga Azam FC akitokea Kagera Sugar aliyochezea msimu uliopita akiwa kama mshambuliaji nyota wa timu hiyo na kinara wa ufungaji mabao akifunga 12 na kufanikisha timu hiyo kumaliza Ligi Kuu katika nafasi ya tatu.

Naye Hoza aliyekuwa kwenye kiwango bora msimu uliopita natokea Mbao FC ya Mwanza.

Azam FC inawatakia kila la kheri wachezaji hao katika maisha yao mapya ndani ya kikosi hicho na inaamini ya kuwa ujio wa nyota hao utazidi kuongeza makali kwenye kikosi hicho kuelekea kwenye changamoto ya kuwania mataji msimu ujao.

Aidha, mbali na benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Mromania Aristica Cioaba, kupendekeza usajili wa nyota hao, tayari ulishafanya uamuzi wa kuwapandisha nyota sita kutoka timu ya vijana ya Azam FC.

Wachezaji hao ni mabeki Abbas Kapombe, Abdul Omary, Godfrey Elias na Ramadhan Mohammed, anayemudu kucheza namba nyingi uwanjani, kiungo Stanslaus Ladislaus na mshambuliaji Yahaya Zaid, aliyeibuka mfungaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza msimu uliopita kwa mabao yake tisa wakati alipokuwa akiichezea kwa mkopo Ashanti United.

Kwa taarifa zaidi za kina, kuhusiana na habari mbalimbali za Azam FC kuelekea kipindi hiki cha usajili, unaombwa kuendelea kufuatilia vyanzo vya rasmi vya habari vya timu hiyo kwenye mtandao wa kijamii wa facebook ‘Azam FC’, instagram ‘azamfcofficial’ na tovuti ya ‘www.azamfc.co.tz’.