MSHAMBULIAJI mpya wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Wazir Junior, amewatoa wasiwasi mashabiki wa timu hiyo akiwaambia kuwa hatowaangusha.

Junior aliyesaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na timu hiyo jana, ameyasema hayo wakati akitambulishwa leo asubuhi na Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd, aliyekuwa sambamba na Meneja wa timu, Phillip Alando na Meneja wa mchezaji huyo, Abdallah Bawazir.

Mshambuliaji huyo amesema kuwa anafurahishwa kujiunga na Azam FC huku akidai zilikuwa ni ndoto zake za muda mrefu kutua kwa mabingwa hao.

“Kwanza namshukuru mwenyezi Mungu kwa kujiunga na Azam FC, pili naishukuru timu yangu ya Toto African niliyocheza misimu miwili, nashukuru ushirikiano wa wachezaji wenzangu pamoja na viongozi na mashabiki, kingine nimefurahi kujiunga na Azam FC,” alisema.

Alisema kuwa anaamini ya timu hiyo ndio mahali pake sahihi kwa kuendeleza kipaji chake huku akidai kuwa itamwezesha kufika mbali kwa kutimiza malengo yake ya kufika mbali yaani kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

“Kwa hiyo nahitaji tu ushirikiano kwa mashabiki na wachezaji wenzangu, mashabiki wasiwe na wasiwasi waje kuisapoti timu yao uwanjani na nawahakikishia sitawaangusha,” alisema.

Kwa upande wake, Jaffar, alisema kuwa wataendelea na zoezi hilo la usajili kwa kusajili wachezaji wengine kwa mujibu wa mapendekezo ya Kocha Mkuu, Aristica Cioaba.

“Kocha ameridhishwa na uwezo wa Wazir (Junior), uongozi ukapambana kuhakikisha unapata saini ya mchezaji huyo na hatimaye tumefanikiwa, ndio kwanza usajili tunauanza, lakini bado hizi ni kama mvua sa lashalasha na masika yanakuja,” alisema.

Mshambuliaji huyo aliyefunga mabao saba msimu uliopita akiwa na Toto African, amekabidhiwa jezi namba saba atakayokuwa akitumia msimu ujao, awali ilivaliwa na mshambuliaji aliyekuwa kwa mkopo Mtibwa Sugar, Kelvin Friday, kabla ya msimu uliopita Shaaban Idd kuitumia kwenye mechi za kimataifa za Kombe la Shirikisho Afrika (CC).