BAADA ya baadhi ya timu kutumia wachezaji waliozidi umri kwenye Ligi ya Azam kwa vijana wenye umri wa miaka 13 (AYLU-13), kamati ya maandalizi ya michuano hiyo imepanga kuhakiki umri kwa timu shiriki ili kuondoa kasoro hiyo.

Michuano hiyo itaendelea kwa wiki ya pili Jumamosi ijayo, Magnet Youth ikicheza na JMK Park Academy saa 3.00 asubuhi, ikifuatiwa na mtanange mwingine baina ya Ilala Academy na Bom Bom FC huku wenyeji Azam FC U-13 wakivaana na Rendis Academy.

Azam FC U-13 ilianza vibaya michuano hiyo kwa kufungwa mabao 4-1 dhidi ya Ilala Academy, huku Rendis nayo ikiichapa Magnet Youth 4-0 na Bom Bom ikiwapepeta JMK Park 4-0.

Akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz Mkuu wa Maendeleo ya Soka la Vijana Azam FC, Tom Legg, alisema kuwa amefurahishwa na namna michuano hiyo ilivyoandaliwa na kila kitu kwenda sawa kwa upande wa wao kama waandaaji.

“Haukuwa mwanzo mzuri kwetu, ila kuna kikubwa cha kujifunza si kwa Azam pekee bali pia kwa timu nyingine, tutahitaji kupitia vitu kadhaa kama vyeti vya kuzaliwa, vitambulisho na hilo nimeliwasilisha kwa baadhi ya makocha wa timu nyingine, hii ni programu endelevu kwa watoto chini ya miaka 17, 15 na 11, hili ni jaribio moja kati ya majaribio mengi yatakayofanyika mwaka huu,” alisema.

Pa kuboresha Azam FC U-13

Legg alisema eneo kubwa la kuboresha kikosi chake ni kufanyia marekebisho eneo la ulinzi na pale wanapokuwa hawana mpira kwani ndio udhaifu uliopelekea kwa kikosi chake kupoteza mchezo wa kwanza.

“Kwa timu ya Azam FC inabidi wafanye kazi kubwa kwenye ulinzi, tunashambulia vizuri lakini linapokuja suala la kukaba hali inakua mbaya hususani tunapocheza bila mpira, lakini ningependa kurudia umuhimu wa michuano hii, suala la kudanganya umri halijengi na itabidi tudhibiti hali hii mapema ili michuano iweze kutoa tunachotarajia,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Ni rahisi kugundua umri wa mchezaji pale anapoingia uwanjani, anavyocheza na umbile na hapo utagundua umri wa mtu, kwa hiyo tutapitia upya majina ya wachezaji na kuhakiki kila mchezaji anakuja mbele, na tunapitia mimi na waandaaji wenzangu.

“Na nimeshawaambia viongozi wa timu nyingine watuletee uthibitisho wa baadhi ya vyeti vya baadhi ya wachezaji, wakituletea itakuwa sawa, wasipoleta basi hawataendelea na mashindano na hii itaendelea kadiri mashindano yanavyoendelea, tukiwa na wasiwasi na umri wa wachezaji tutaomba vidhibiti wasipotupatia tunawaondoa.” alimalizia kwa msisitizo mtaalamu huyo kutoka nchini England.

Wakati michuano hiyo ikitarajia kuhitimika Julai 29 mwaka huu, mpaka sasa kwenye msimamo wa ligi hiyo vinara ni Bom Bom, Rendis na Ilala kila mmoja akiwa amejikusanyia pointi tatu, huku Azam FC U-13 ikifuatia katika nafasi ya nne ikiwa haina pointi yoyote sawa na JMK Park na Magnet Youth zinazofuatia kwenye nafasi ya tano na sita.