MICHUANO ya vijana chini ya umri wa miaka 13 ya Azam (Azam Youth U-13), imeanza rasmi leo kwa timu zote sita kuchuana ndani ya Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Timu hizo zinazoshiriki michuano hiyo ni wenyeji Azam FC U-13, Rendis Academy U-13, JMK Park Academy U-13, Magnet Youth U-13, Bom Bom SC U-13 na Ilala Academy U-13, ambazo zitakuwa zikipapatuana katika wiki 10 za mashindano hayo hadi Julai 29 mwaka huu.

Wenyeji wa Azam FC U-13 wameanza vibaya michuano hiyo kwa kufungwa mabao 4-1 dhidi ya Ilala Academy, huku Rendis nayo ikiichapa Magnet Youth 4-0 na Bom Bom ikiwaua JMK Park 4-0.

Kwa mujibu wa matokeo hayo vinara wa ligi hiyo ni Bom Bom, Rendis na Ilala kila mmoja akiwa amejikusanyia pointi tatu, Azam FC ambayo haijavuna pointi yoyote inafuatia katika nafasi ya nne sawa na JMK Park na Magnet Youth zinazofuatia kwenye nafasi ya tano na sita.

Mashindano hiyo ya aina yake yenye burudani kutoka kwa vijana wadogo, itaendelea tena Jumamosi ijayo Juni 3 mwaka huu katika uwanja huo.