KIPA Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu na nyota wa Azam FC, Aishi Manula, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kufuatia taarifa zinazoenezwa kuwa tayari amesaini Simba kwa ajili ya msimu ujao.

Kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram, Manula amewaambia mashabiki wa timu hiyo kuwa bado ana mkataba na Azam FC utakaomalizika Julai mwaka huu, na hivi sasa yupo kwenye mazungumzo na viongozi wa Azam FC juu ya kuuongeza.

Kipa huyo namba moja wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, ameweka wazi kuwa mazungumzo hayo yanaendelea vizuri na anaamini atasaini katika timu hiyo iliyomtunza na kumlea vema hadi leo hii kuanzia kwenye academy yake hadi timu kubwa, hivyo kuwatoa hofu kabisa mashabiki baada ya kupokea simu nyingi wakimuuliza juu ya kusaini Simba.

Unaweza kuusoma ujumbe wake wote kupitia picha iliyoambatanishwa na stori hii.