WINGA wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, aliyeko kwa mkopo kwenye timu ya CD Tenerife ya Hispania, Farid Mussa, tayari amemaliza msimu akiwa katika timu ya vijana huku mambo yakionekana kumwendea vema baada ya kufanya vizuri.

Farid alijiunga na kikosi cha timu hiyo Desemba mwaka jana baada ya kumaliza taratibu zote za kujiunga na Tenerife, ambayo kwa sasa inapigana kwenye mechi za mwisho za mtoano (play off) ili kupata nafasi ya kupanda katika Ligi Kuu Hispania (La Liga).

Farid ameuambia mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa kwa sasa amezoea kabisa soka la kihispania kufuatia kupata tabu kuzoea hapo awali alipokwenda kujiunga nao.

“Mwanzo ilikuwa ngumu kwa kweli kwangu, kwanza kutofanya mazoez na timu kwa muda wote niliokuwa Tanzania wakati uhamisho wangu ukishughulikiwa na pili kutocheza mechi kuliniathiri kabisa.

“Kwa hiyo ilikuwa ngumu kuonyesha uwezo wangu niliokuwa nao kipindi kile, ila nashukuru nilivyokuja timu ya Taifa na kucheza mechi zile mbili dhidi ya Botswana na Burundi, na nilivyorudi Hispania nikabadilika kupita maelezo, kwani kwa kiasi fulani mechi hizo ziliniongezea hali ya kujiamini,” alisema.

Kuhusu kupandishwa timu ya wakubwa kwa ajili ya msimu ujao, suala hilo litaamuliwa na kocha wa timu ya vijana, Quico de Diego, atakapowasilisha ripoti yake kwa Kocha Mkuu wa wakubwa, Jose Luis Marti.

Rekodi alizomaliza nazo

Timu ya vijana ya CD Tenerife iliyokuwa ikishiriki Ligi Ngazi ya Nne nchini Hispania ‘Tercera Division’ kanda ya Visiwa vya Canary, imemaliza katika nafasi ya tano huku Farid, akiwa ni mmoja wa wachezaji wa kikosi hicho waliofanikisha mafanikio hayo.

Hadi anamaliza msimu Mei 13 mwaka huu kwa Tenerife kuwachapa El Cotillo mabao 3-2, Farid alitupia bao moja dakika ya 80 na kuhitimisha msimu kwa rekodi ya aina yake.

Winga huyo ambaye amebadilishwa namba kutoka namba 11 aliyozoea kucheza kipindi cha nyuma na sasa mara nyingi akicheza upande wa kulia (7), amefanikiwa kucheza mechi 13 na kufunga mabao sita na kutoa pasi za mwisho sita zilizozaa mabao (assist).

Mafanikio ya Farid kwa kiasi kikubwa yameibeba timu yake hiyo, kwani wakati anajiunga nao aliikuta nafasi ya 14 kwenye msimamo, lakini ikafanya vizuri zaidi na kumaliza nafasi ya tano mwishoni mwa msimu.