HAFLA ya utoaji tuzo kwa wachezaji bora waliofanya vizuri kwenye Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2016/17 uliomalizika wikiendi iliyopita, inatarajia  kufanyika kesho Jumatano Mei 24 mwaka huu katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Katika tukio hilo, wachezaji watatu wa kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, wanatarajia kuwa miongoni mwa nyota watakaowania tuzo katika vipengele mbalimbali vilivyoainishwa, ambao ni kipa bora kwa sasa nchini Aishi Manula na makinda wawili, mshambuliaji Shaaban Idd na kiungo Abdallah Masoud ‘Cabaye’.

Manula ambaye pia ni kipa namba moja wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, atakuwa akiwania tuzo mbili tofauti, ya kwanza ikiwa ni ya Mchezaji Bora wa msimu na nyingine ni Kipa Bora wa msimu.

Hadi msimu unamalizika, kipa huyo amefanikiwa kudaka kwenye mechi 29 kati ya 30 za msimu (sawa na dakika 2,610) zikiwa ni nyingi kuliko kipa mwingine yoyote VPL, kati ya hizo ameiongoza Azam FC kutoruhusu kufungwa bao (cleansheet) katika michezo 15 (sawa na dakika 1,350).

Shaaban Idd aliyefunga mabao saba kwenye Ligi Kuu msimu huu baada ya kucheza dakika 891, amekuwa na wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 127.28, ameteuliwa kuwania tuzo ya Mchezaji Bora Anayechipukia baada ya kufanya vizuri msimu huu.

Kiungo ambaye bado hajapata namba ya uhakika kwenye kikosi cha kwanza cha Azam FC, Abdallah Masoud, ameteuliwa kuwania tuzo ya Mchezaji Bora wa michuano ya Ligi ya Vijana iliyomalizika Desemba mwaka jana, tuzo iliyopewa jina ya mchezaji wa Mbao aliyefariki uwanjani, Ismail Khalfan ‘Tuzo ya Ismail Khalfan U-20’.

Orodha ya Tuzo na Wanaowania:

MCHEZAJI BORA:

-Aishi Manula (Azam FC)

-Simon Msuva (Yanga)

-Shiza Kichuya (Simba)

-Haruna Niyonzima (Yanga)

-Mohammed Hussein (Simba).

(Majina ya wanaowania tuzo hiyo yalitolewa Jumatano iliyopita, na upigaji kura unaendelea ukiwahusisha Makocha wa timu za Ligi Kuu na Makocha Wasaidizi,Wahariri wa habari za michezo na Manahodha wa timu za Ligi Kuu, ambapo mwisho wa kufanya hivyo ni Jumanne Mei 23 mwaka huu).

KIPA BORA:

-Aishi Manula (Azam FC)

-Owen Chaima (Mbeya City)

-Juma Kaseja (Kagera Sugar).

KOCHA BORA:

-Joseph Omog (Simba)

-Mecky Mexime (Kagera Sugar)

-Ettiene Ndayiragije (Mbao).

MWAMUZI BORA:

-Shomari Lawi (Kigoma)

-Elly Sasii (Dar es Salaam)

-Hance Mabena (Tanga)

MCHEZAJI BORA WA KIGENI:

-Haruna Niyonzima (Yanga)

-Method Mwanjali (Simba)

-Yusuph Ndikumana (Mbao)

MCHEZAJI BORA ANAYECHIPUKIA:

-Mbaraka Abeid (Kagera Sugar)

-Shaaban Idd (Azam FC)

-Mohammed Issa (Mtibwa Sugar)

TUZO YA ISMAIL KHALFAN U-20:

-Shaaban Idd (Azam FC)

-Abdallah Masoud (Azam FC)

-Mosses Kitambi (Simba)

TUZO YA HESHIMA:

-Atatangazwa aliyeteuliwa siku ya hafla ya tuzo hizo.

GOLI BORA LA MSIMU:

-Tayari kuna mabao bora 10 ambayo yataoneshwa siku hiyo ukumbini ikiwemo lile bora la msimu mzima.

TIMU YENYE NIDHAMU:

-Mshindi atatangazwa ukumbini siku hiyo kulingana na vigezo vilivyopo.

WACHEZAJI 11 BORA WA MSIMU:

-Watatangazwa ukumbini siku hiyo ya hafla.